May 8, 2013

Bomu Arusha: Pengo afichua siri

Kadinali Pengo 

Dar es Salaam/Arusha. Kadinali Pengo alisema amepata taarifa kutoka kwa watu ambao hana na shaka nao.
“Jumapili, niliongelea kwamba suala zima la tukio la Arusha halihusiani na imani yoyote ya kidini. Tamko hilo nilitamka kutokana na taarifa nilizofikishiwa na watu ambao sikuweza kuwa na shaka kwamba wanaoniambia ni kweli na sidhani kama ningekuwa na sababu ya kusema wamefika kwa kunidanganya kwa hiyo tamko litakuwa limesimama juu ya msimamo huo,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza:
“Lengo la msingi kabisa, langu na la kanisa ni kwamba tukio lolote lile liwe kwa nia mbaya au nzuri kwa upande wetu isiwe ni sababu ya kuanza mapambano na kuwa chimbuko la ukosefu wa amani katika nchi yetu,” alisema Pengo.
Alisema kuwa kila anayehusika ajue amani ya kweli ya taifa lolote haiwezi ikapatikana isipokuwa ikijengwa juu ya ukweli na ukweli kabisa bila kufuta au kujaribu kupotosha ukweli kwa namna yoyote ile.
“Tusipojua kusema ukweli ulivyo hatuwezi kufaulu kuleta amani katika taifa letu. Kwa hiyo pamoja na kuendelea kuwaomba waumini wa Katoliki pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu arehemu taifa letu na mapambano ya aina yoyote ile. Tuendeleze nia yetu njema ya kusema ukweli, haidhuru ukweli huu unamgusa nani,” alisema Pengo.
Alisema kujaribu kuficha ukweli na kupotosha ni njia sahihi kwa ibilisi kuleta vurugu katika jumuiya ya watu na ieleweke hivyo.
“Naomba kila mtu akubaliane na tamko langu haidhuru pana kosa, amani ya taifa letu ni jambo la msingi na amani itajengwa tu iwapo kila mtu anayehusika atakuwa tayari kusema ukweli kama ulivyo,” alisema.
Mwingine afariki, 20 wakutwa na vipande vya chuma miilini

Katika hatua nyingine, majeruhi mmoja katika shambulio hilo lililotokea Jumapili iliyopita, amefariki dunia juzi jioni na kufikisha idadi ya waliopoteza maisha kufikia watatu.
Aliyefariki ni mtoto wa miaka tisa, Patricia Joachim ambaye alikuwa amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi. Wengine waliofariki katika tukio hilo ni Regina Losyoki (45) na James Gabriel (16).
Mazishi ya watu hao watatu yamepangwa kufanyika katika eneo la kanisa hilo Ijumaa.
Katika hatua nyingine, majeruhi 20 wamebainika kuwa na chembechembe za vyuma walivyopata katika shambulio hilo. Hao ni miongoni mwa majeruhi 42 waliolazwa hadi sasa kwenye hospitali mbalimbali za Arusha.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Thomas Kway alisema majeruhi hao 20 wamedhuriwa na chembechembe za vyuma vya mabomu na baada ya miili yao kubainika kuwa na vyuma vyenye urefu hadi wa sentimita tisa.
Dk Kway alisema hayo wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipofika katika hospitali hiyo kuwafariji majeruhi hao.

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliwataka madaktari waliowafanyia upasuaji majeruhi waliolipuliwa na bomu kuhifadhi vipande hivyo ili vitumike katika uchunguzi.
Aliwaambia wabunge kuwa vyuma hivyo vitasaidia upelelezi ili kufahamu aina ya bomu lililotumika.
“Tumeamua kuwa vipande vya vyuma vinavyotolewa baada ya upasuaji visitupwe, vitumike kwa uchunguzi,” alisema Pinda na kuongeza kuwa baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Waliokamatwa
Akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alifika Arusha jana, Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema watu tisa wamekamatwa hadi sasa.
Aliwataja baadhi yao kuwa ni Victor Ambrose na wengine aliowataja kwa jina mojamoja ni Joseph na David.
Alisema wengine ni raia watatu wa Saudi Arabia, ambao walikuwa na wenyeji wao wawili na Watanzania wengine watatu.
Kauli ya Kikwete
Akizungumza Arusha jana, Rais Kikwete amewataka waumini wa dini zote waendelee kusali akiahidi kwamba Serikali itaimarisha ulinzi. Alisema amekerwa na kukasirishwa na tukio hilo.
Rais Kikwete alitanguliwa kufika Arusha na Makamu Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ambao pia walitembelea Kanisa lililolipuliwa na baadaye kwenda kuwatembelea wafiwa na kuwafariji majeruhi hospitali.
Viongozi wote hao walitoa wito kwa Watanzania kulinda amani iliyopo na kuacha malumbano ambayo hayana tija kwa maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...