Waandishi wa habari wakiandamana kuelekea kwenye viwanja vya
Jangwani jijini Dar es Salaam asubuhi ya leo.
|
Waandishi wa habari wakiandamana kuelekea kwenye viwanja vya
Jangwani jijini Dar es Salaam asubuhi ya leo.
|
Mojawapo ya mabango yaliyokuwapo kwenye maandamano ya waandishi wa habari ya kupinga mauaji ya mwandishi mwenzao kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam asubuhi ya leo. |
Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena akihutubia waandishi wa
Habari walioandamana.
|
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, amekumbana na fadhaa
ambayo haikutarajia wakati alipotimuliwa katika maandamano ya waandishi wa
habari ya kupinga mauaji ya mwandishi mwenzao wa kituo cha televisheni cha
Channel Ten, David Mwangosi, wakati alipozuka bila mwaliko.
Huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti, waandishi
waliandamana kuanzia kwenye ofisi za Channel Ten katikati ya jiji la Dar es
Salaam na kutembea hadi katika viwanja vya Jangawani lakini walipofika mwisho
wa maandamano yao walipigwa na butwaa baada ya kumkuta Waziri Nchimbi akiwa wa
kwanza kufika katika eneo hilo tayari kupokea maandamano.
Wakati Nchimbi akijiandaa kuanza kuzungumza mbele ya wanahabari,
upinzani mkali ukazuka kwa waandishi dhidi ya kiongozi huyo wa serikali wakitaka
aondoke mahala hapo kwani maandamano hayo yalikuwa hayamuhusu.
"Atokee.... aondokee.... hatumtakiiii.... nani kamleta
hapa?" yalikuwa ni baadhi ya maneo yaliyokuwa wakitolewa kwa sauti kubwa
kupinga uwapo wa waziri Nchimbi mahala hapo.
Huku akizomewa, Waziri Nchimbi alijaribu kuvumilia aibu hiyo kwa
takriban dakika tano huku pengine akitumai kwamba watamruhusu kuzungumza
kilichompeleka mahala hapo.
Mwandishi wa habari mkongwe, ambaye pia ni mwanasheria, Nyaronyo
Kicheere, alisogea mbele ya umati wa waandishi na kusimama jirani na
alipokuwapo waziri Nchimbi na kusema: "Tumeambiwa tunakuja hapa kwa ajili
ya mkutano wa waandishi wa habari na utapokewa na jukwaa la wahariri, inakuwaje
tupokewe na mtu mwingine. Hatumhitaji mtu mwingine hapa, aondoke."
Baada ya kauli hiyo, waziri Nchimbi aliondoka mahala hapo na
kuzua shangwe kubwa kwa waandishi ambao pia walimsindikiza kwa kumzomea mpaka
alipoingia katika gari lake la wizara. Hakuja na gari lake la waziri.
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walizungumza na kukemea
mauaji hayo na bila ya kuuma-uma maneno walisema kwamba Mwangosi aliuawa kwa
kulipuliwa na polisi na kwamba waliohusika wote wachukuliwe hatua za kisheria.
"Waandishi na wafanyakazi wengine wanalipa kodi ilipolisi
wapate magwanda, wapate bunduki, wapate mabuti na wanalipwa ili walinde raia na
sio kuua raia, vitendo kama hivi havikubaliki," alisema Jesse Kwayu,
mhariri mkuu wa gazeti la NIPASHE.
Mwandishi mkongwe, Masoud Sanani, aliongeza: "Waarabu
wanasema 'wal kiswaswa haq' yaani 'kisasi ni haki', lakini sisi kwa busara
tunasema kwamba hatuna kisasi ila tunataka mambo haya yawe mwisho, waandishi
waachwe wafanye kazi zao kama askari wanavyoachwa wafanye kazi zao."
"Tumeshasikia askari akitingishwa kidogo, mtu anashitakiwa
kwa kumzuia askari kufanya kazi yake, tunataka waandishi nao waachwe wafanye
kazi yao," alisema.
Waandishi walitaka familia ya marehemu Mwangosi ilelewe na
watoto wasomeshwe mpaka watakapofikia.
Miongoni mwa mabango yaliyokuwapo katika maandamano hayo
yalisomeka: "Bunduki na mabomu hayatazuia kalamu zetu kuandika
ukweli," "Hatuogopi vitu vizito wala vitu vya ncha kali"....
Yalikuwa
ni maandamano ya amani. Hapakuwa na vurugu zozote na askari waliokuwapo wengi
walikuwa mikono mitupu bila ya silaha yoyote hata virungu ukiacha wachache
waliobeba silaha na askari wa usalama barabarani waliongoza maandamano wakizuia
magari wakati waandishi wakipita katika njia zote kuelekea kwenye viwanja vya
Jangawani.
No comments:
Post a Comment