Aug 9, 2012

Ndege za Malawi zafungasha virago Ziwa Nyasa...

Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe

SIKU chache baada ya Serikali kuzitaka ndege zinazozunguka Ziwa Nyasa upande wa Tanzania kufanya utafiti wa mafuta kuondoka mara moja, Serikali ya Malawi imetii na kuziondoa kampuni zinazofanya kazi hiyo katika ziwa hilo.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake Jumatatu iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliitaka Malawi kuziondoa ndege na kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta katika eneo hilo kwa kuwa ni mali ya Tanzania.

Mbali na Waziri Membe, viongozi wengine waliozungumzia mgogoro huo na kuitaka Malawi iache uchokozi ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa.

Wakati Sitta akiwataka Watanzania kuendelea na shughuli zao bila hofu kwa kuwa Serikali iko tayari kwa tishio lolote, Lowassa alisisitiza kuwa Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia
vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo.

Jana kwa nyakati tofauti, Wakuu wa Wilaya nne zilizo mpakani mwa Tanzania na Malawi za Ileje, Mbozi, Mbeya, Kyela na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro walieleza kuwa mara baada ya kauli hizo, ndege hizo za Malawi ziliondoka na kampuni zilizokuwa zikitafiti mafuta katika Ziwa Nyasa zimeacha.
“Hapa tuko cool (tulivu) kabisa tangu zile ndege zilipoacha kuruka, tofauti na hizo kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali (ya Malawi),” alisema Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk Michael Kadeghe na kuongeza:

“Hapa niko kwenye Sherehe za Nanenane na Malawi wana banda lao nimetoka kulitembelea. Hali iko shwari, tunaendelea na uhusiano kama kawaida.”

Kuhusu mradi wa Bonde la Mto Songwe unaozihusisha Wilaya za Mbozi, Ileje, Rungwe, Mbeya Vijijini na Malawi, Dk Kadeghe alisema bado haujaathirika.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, Norman Sigalla alisema mgogoro huo kwa sasa uko kwenye hatua za awali hivyo ni vigumu kusema kuwa nchi inaweza kuingia vitani au la.
Kuhusu Mradi huo wa Bonde la Mto Songwe, Sigalla alisema bado haujaathirika kwa kuwa hakuna aliyekiuka makubaliano.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Sengamule alisema: “Hapa kwetu tuko shwari kabisa, hata juzi nilikuwa na viongozi wa Malawi waliokuja hapa kwa ajili ya Mradi wa Bonde la Mto Songwe tukajadiliana jinsi ya kuuendeleza. Hata jana nimepita eneo la mpakani sijaona tishio lolote, labda huko Kyela.”

Kwa upande wake, Kandoro alisema: “Mimi naona tuko shwari, hakuna tishio lolote. Nadhani ulimsikia juzi Waziri wa Mambo ya Nje akisema. Tuache diplomasia ifanye kazi yake. Uhusiano wetu wa kidiplomasia na Malawi haujaharibika.”

Kyela kazi kama kawaida

Wakazi wa Kyela wakiwamo wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Nyasa wamesema wanaendelea na kazi zao za kila siku kama kawaida licha ya kuibuka kwa mgogoro huo wa mpaka.

Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema licha ya kusikia mgogoro huo, bado wameendelea kuwa na uhusiano mzuri kati yao na Wamalawi.

Walisema kuwa tangu kuibuka kwa mjadala kuhusiana na mpaka huo wa Ziwa Nyasa, hakuna tatizo ambalo limeonekana miongoni mwao na kwamba muda wote wanaendelea na shughuli zao za mpakani.

Mkazi wa Kata ya Kabanga Songwe, Lusajo Mwakapisu alisema hakuna tukio lolote ambalo limeweza kuripotiwa kuhusiana na mgogoro unaoendelea baina ya nchi hizo mbili.

Alisema wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na hakuna kizuizi chochote mpakani mwa Tanzania na Malawi na kwamba muda wote wamekuwa wakivuka mpaka na kuingia nchi hiyo jirani.

Wavuvi katika ziwa hilo walisema muda wote wapo kazini na hakuna kikwazo chochote kwao tangu kuripotiwa kwa mgogoro huo.

“Sisi hapa kama unavyoona mwenyewe tunaendelea na kazi yetu ya uvuvi kila siku. Hakuna mgeni yeyote aliyeonekana kuja na kutusemesha lolote kuhusiana na mgogoro huo,”  alisema mvuvi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joseph.

Kiini cha Mgogoro

Waziri Membe akizungumzia kiini cha mgogoro huo,  alisema ni hatua ya Serikali ya Malawi kushikilia msimamo kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi wakati Tanzania inasema mpaka upo katikati ya Ziwa.

“Wenzetu wanadai ziwa lote lipo Malawi lakini, nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati,” alisema.

Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwapo baina ya Cameroon na Nigeria. Alisema katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Dunia, iliamuliwa kuwa mpaka baina ya nchi hizo mbili upite katikati ya Ziwa Chad ukifuata msitari ulionyooka.

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...