Rais John Atta Mills |
Rais John Atta Mills wa Ghana amefariki dunia
ghafla jana kutokana na kuugua. Kufuatia kifo hicho, makamu wa Rais ameapishwa
mara moja kushika wadhifa huo. Serikali imetangaza wiki moja ya maombolezo
kitaifa.
Mills aliyekuwa
na umri wa miaka 68 amefariki ikiwa ni miezi michache kabla ya kushiriki tena
kwenye uchaguzi wa Urais utakaofanyika mwezi Desemba mwaka huu. Mills alikutwa
na mauti akiwa hospitalini kwenye mji mkuu wa nchini hiyo Accra alipokuwa
anapatiwa matibabu.
John Dramani Mahama, (katikati) rais mpya
wa Ghana akiwa na viongozi wenziwe
|
Katika siku za
hivi karibuni alikwenda Marekani kwa ajili ya kupima afya yake. Sababu za kifo
chake bado hazijajulikana. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Makamu wa Rais
John Dramani Mahama ndiye amechukua nafasi na tayari ameshaapishwa. Ghana,
taifa la Afrika ya Magharibi inasifiwa kuwa kitovu cha demokrasia.
Mahama alikula
kiapo mbele ya bunge la dharura lililoitishwa mara baada ya kifo hicho na
ameahidi kulinda amani na utulivu wakati wote atakaokuwa madarakani kumalizia
muhula wa mtu aliyemrithi.Tayari kiongozi huyo mpya ameshatangaza wiki nzima ya
maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti. Ana umri wa miaka
53 na alikuwa waziri wa mawasiliano kabla ya kushika wadhifa wa makamu wa Rais.
Katiba hotuba yake mara baada ya kiapo Mahama alisema amepoteza mtu muhimu
sana.
Mataifa yatuma rambirambi
Viongozi
mbalimbali wametoa salamu za rambirambi akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani.
Obama aliichagua Ghana kuwa nchi ya kwanza kuitembelea kusini mwa jangwa la
Sahara baada ya kuchukua majukumu ya urais mwaka 2009. Katika taarifa yake
rasmi, amemuelezea Marehemu Mills kuwa ni mtu aliyepigana bila kuchoka kuinua
maisha ya Waghana. Viongozi wengine wa mataifa ya Nigeria, Cote d'Ivoire na
Togo pia wametoa rambirambi zao. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon,
naye ameusifu uongozi wake.
Rais Barack Obama wa Marekani na
Marehemu John Atta Mills Ghana
|
Uvumi kuhusu maradhi yake
Vituo vya
televisheni nchini Ghana GTV na TV3 vilisitisha matangazo yake ya kawaida
kutangaza habari za kifo cha kiongozi huyo hapo jana. Maafisa wa serikali
hawajatoa sababu za kifo chake ambacho kimemkuta siku tatu baada ya
kusheherekea siku yake ya kuzaliwa.
Taarifa ya
kuzorota kwa afya yake zilienea kufuatiwa safari za mara kwa mara alizofanya
kwenda Marekani. Hata vyombo vya habari vya upinzani viliripoti kuwa hana uwezo
wa kushiriki uchaguzi wa duru ya pili hapo mwezi Desemba. Taarifa ambazo hazina
uthibitisho kutoka vyombo vya habari vya ndani ya nchi hiyo zinasema kuwa
maradhi ya saratani ya koo ndiyo yaliyomuuwa.
Marehemu Mills
aliwahi pia kuwa makamu wa Rais chini ya utawala wa Jerry Rawlings kiongozi wa
mapinduzi ambaye baadae alichaguliwa kushika madaraka kwa kura nyingi.
Aliushangaza ulimwengu kwa kuachia ngazi baada ya uchaguzi wa mwaka 2000.
Chanzo: Deutsche Welle
No comments:
Post a Comment