Dr Slaa na Mkewe mtarajiwa Josephine Mushumbusi |
ROSE
KAMILI AFUNGUA KESI KUZUIA ASIFUNGE NDOA KANISANI JULAI 21, MWENYEWE
ASEMA HIZO NI SIASA
ROSE
Kamili anayedai kuwa ni mke wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa,
amefungua kesi Mahakama Kuu akiiomba isimamishe ndoa ya kiongozi huyo na mke
mwingine inayotarajiwa kufungwa Julai 21, mwaka huu wilayani Karatu Mkoa wa
Manyara. Dk Slaa anatarajia kufunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi,
Josephine Mushumbusi.
Kamili
ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), pia anaiomba Mahakama iamuru Dk
Slaa amlipe Sh50 milioni za fidia aliyotumia kujihudumia pasipo matunzo ya
mumewe huyo.
Mbunge
huyo kupitia kwa Wakili wake, Joseph Thadayo, aniomba pia Mahakama iamuru
Mushumbusi amlipe kiasi cha Sh500 milioni za fidia ya maumivu aliyoyapata
kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Kesi hiyo
namba nne ya mwaka 2012 iliyopangwa kusikilizwa na Jaji Lawrance Kaduli,
inatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza leo. (Jumatano)
Katika
hati hiyo ya madai, mbunge huyo anadai kuwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kati ya
Dk Slaa na Mushumbusi ni batili kwa sababu kuna ndoa nyingine halali na
inayoendelea kuishi kati ya Slaa na Kamili iliyofungwa mwaka 1985.
Alidai
baada ya kufugwa kwa ndoa hiyo, Juni 18, 1987 walifanikiwa kupata mtoto wa kike
anayeitwa Emiliana Muchu na baadaye Septemba 23, 1988 walipata mtoto mwingine
wa kiume, Linus Amsi.
Katika
uhusiano wao, Dk Slaa akiwa ni Padri wa Kanisa Katoliki, alifanya taratibu
zilizomwondosha katika nafasi hiyo na kuanza maisha ya familia.
Baada ya
taratibu hizo, jamii ya Watanzania iliwatambua kama mume na mke na hata
kumbukumbu za hati za kimataifa kama za kusafiria ziliwatambua kuwa wanandoa.
Kamili
aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa yeye na Slaa waliishi maisha ya ndoa
yenye amani yaliyowawezesha kupata mali kadhaa walizomiliki kwa pamoja ikiwemo
nyumba iliyopo kwenye Kiwanja namba 609 Kitalu E iliyopo Sinza, Dar es Salaam,
nyumba ya makazi iliyopo Kijiji cha Gongali huko Karatu na vifaa mbalimbali vya
nyumbani.
Hati ya
mashtaka imeendelea kudai kuwa uhusiano kati ya Slaa na Kamili, ulianza
kuharibika mwaka 2009, baada ya mume huyo kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine
kinyume cha sheria… “Tangu mwaka huo 2009, Slaa akaitelekeza familia yake kwa
kutoipatia huduma,” imeeleza hati hiyo.
Kamili
anaiomba Mahakama iamuru kuwa yeye na Dk Slaa bado ni mke na mume na kwamba
Mushumbusi aliingilia ndoa yao hivyo izuie ndoa inayotarajiwa kufungwa Julai
21, mwaka huu huko Karatu, Manyara.
Kamili
pia amewasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo
akimweleza Askofu Mkuu huyo wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam kuwa moja ya
Parokia za Dar es Salaam zina taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya
madai hayo pia imewasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Msajili wa Ndoa na
kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbulu.
Katibu Mkuu
wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa
|
Dk Slaa:
Nimeyazoea
Alipotakiwa
kuzungumzia kesi hiyo nje ya Mahakama, Dk Slaa alisema: “Hayo mambo nimeyazoea
na kimsingi hayanipi shida yoyote.”
Alipoulizwa
endapo anajipanga vipi kulipa fidia hiyo alijibu: “Kesi ni kesi hivyo siyo kila
kinachoombwa kwenye kesi lazima kilipwe.”
Hata
hivyo, Dk Slaa alisema asingependa kuzungumzia suala hilo kwa undani kwa kuwa
liko kwa mawakili wake lakini akasema amebaini kuwa hizo ni hila na michezo
michafu ya kisiasa.
“Kwanza
siyo pingamizi moja tu, kuna pingamizi mbili mahakamani lakini kwa ufupi
ifahamike kuwa hizo ni hila.”
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment