Rais JK Kikwete |
ASEMA MADAKTARI WASIOKUBALI MSHAHARA WA SERIKALI
WAFUNGASHE VIRAGO
Boniface Meena (Gazeti la Mwananchi)
WAKATI Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania,
Dk Steven Ulimboka akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete
amesema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa
kiungo muhimu katika majadiliano baina ya pande hizo mbili.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake
ya kila mwezi, ambapo mbali na suala hilo, pia alizungumzia sababu za mgomo wa
madaktari na usafirishaji wa wahamiaji haramu.
Dk Ulimboka ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa
madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali kushindwa kutimiza madai
yao mbalimbali, anatibiwa figo na majereha aliyoyapata katika sehemu mbalimbali
za mwili, baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa
kucha, meno mawili na kutupwa katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano
iliyopita.
Tangu kutokea kwa unyama huo uliofanywa na watu
wasiojulikana, baadhi ya wananchi na wanaharakati wamekuwa wakiilaumu Serikali
kuwa inahusika na utekaji huo na wengine wakienda mbali zaidi, kuwa watekaji
walikuwa wanamlazimisha kueleza nani yuko nyuma ya mgomo wa madaktari.
Rais Kikwete, kama awali alivyosema Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, walisema wanatambua kuwa, Serikali nayo inatajwa katika orodha
ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini yeye ameshangazwa
na hisia hizo, kwani haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
"Dk Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika
mazungumzo baina ya Serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa
Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na
rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini
kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali,"
alisema Rais Kikwete.
Alisema Serikali haina sababu ya kumdhuru Dk
Ulimboka kwa sababu suala la mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya
kuusitisha, hivyo anayekaidi amri hiyo atakuwa ananunua ugomvi na mhimili huo
wa dola, ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu.
"Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na
ugomvi na Dk Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue
kumdhuru?" alihoji na kuongeza:
"Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa
kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali,"
alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk Ulimboka kimemsikitisha na
kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na
desturi za Tanzania.
Alisema Watanzania hawajazoea mambo hayo na kwamba
ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli
ujulikane.
"Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane
mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea
hivi sasa," alisema.
Alisema anatoa mkono wa pole kwa Dk Ulimboka na
kumwombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika
ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete pia alimpongeza Juma Mgaza ambaye
alimsaidia Dk Ulimboka kumtoa katika pori alikotupwa na kumpeleka kituo cha
polisi kwa moyo wake wa huruma.
Kuhusu mgomo
Kuhusu mgomo unaoendelea Rais Kikwete alisema,
kiwango cha mshahara cha Sh3.5 milioni wanachokitaka madaktari Serikali haina
uwezo wa kukitoa, hivyo daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini
bila ya kulipwa mshahara huo, awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri
anayeweza kumlipa kiasi hicho.
Rais Kikwete alisema, kwa sasa Serikali haiwezi
kuwaahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa Sh3.5 milioni na
posho zote zile, kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa
Sh7.7 milioni kwa mwezi, kitu ambacho haitakiweza.
"Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu
tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari. Kutokana na ukweli huo
basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa
mshahara huo awe huru kuacha. Nasi tutamtakia kila la heri,"alisema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete alisema, madaktari hawana sababu ya
kugoma ili washinikize kulipwa mshahara huo kwani uwezo haupo.
"Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na
kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote
hayo kwa kujiondoa mwenyewe," alisema.
Alisema mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua
hizo kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria za kazi na wataendelea kufanya
hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.
Alisema anajua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna
manun’guniko ya kuonewa yatajitokeza, lakini ni bora kufanya hivyo ili
ijulikane Serikali haina daktari.
"Mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya
hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na
huyo anayekuja awe na mahali pa kuishi."
Kutokana na hali hiyo amewasihi madaktari kuacha
mgomo na kurejea kazini, kwani Watanzania wanateseka na kupoteza maisha.
Sababu za mgomo
Rais Kikwete alisema kwamba, kuna masuala matatu
ambayo yamekuwa na mwafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo
kati ya madaktari na Serikali.
Alisema suala la kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi ambalo Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya
kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
Pia alisema Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha
posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili na utekelezaji
wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni
yapi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.
Rais Kikwete alisema kuwa, madaktari wamekataa
suala hilo la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao,
yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
Alisema suala la pili ambalo wamekubaliana nusu
nusu ni kuhusu nyumba za kuishi ambalo Serikali imekiri wajibu wake wa
kuwapatia nyumba za kuishi.
Rais Kikwete aliongeza kwamba, kwa maeneo ambayo
madaktari wanalipwa posho ya pango, Serikali imesema waajiri wataendelea
kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye
stahili ya kupewa nyumba.
Alisema jambo hilo limekataliwa na madaktari na
kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba, Serikali kwa
upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa kama
wafanyakazi wengine wote wa umma.
Alisema suala lingine ambalo lilikuwa na
makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira
magumu na pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini
yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma, hivyo hatua zichukuliwe
kuwasaidia watumishi hao.
Kuhusu posho, alisema Serikali imekubali kuwapo
posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha
mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Alisema madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la
uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.
"Tofauti hapa si posho hiyo kuwapo, bali ni
rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango
vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya
kufanya hayo," alisema.
Alisema kuna mambo mawili ambayo hayakuwa na
mwafaka kabisa kati ya pande hizo mbili na la kwanza ni posho ya kuitwa kazini
(on call allowance).
Rais Kikwete alisema, Serikali ilishaongeza posho
hizo tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa
daktari bingwa, Sh20,000 kwa dakari mwenye usajili wa kudumu na Sh15,000 kwa
madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns).
Alisema hata hivyo, madaktari kwa upande wao
hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya
mshahara.
Rais Kikwete alisema ugumu wa kukubali pendekezo la
madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini na kwamba ukitaka
ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa
au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
Alisema jambo la pili ambalo mwafaka haukufikiwa
baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari
ambao madaktari wanataka uwe Sh3.5 milioni wakati Serikali inasema kiasi hicho
hatukiwezi.
Alisema Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza
mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi
wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.
Rais Kikwete alisema, kwa kiwango cha sasa cha
mshahara wao, daktari ataanzia kati ya Sh1.1 milioni na Sh1.2 milioni kutegemea
kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.
"Madaktari wamekataa katakata na
wameng’ang’ania Sh3.5 milioni," alisema.
Alisema ni muhimu madaktari wakatambua kuwa
wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo usiokuwa halali
kisheria ambao pia haustahili kuwapo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.
Alisema viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza
madaktari katika mgogoro na mahakama na waajiri wao isivyostahili.
Rais Kikwete alisema ni vyema viongozi wa madaktari
na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia
kiongozi wao mkuu amekana mahakamani kuwa hahusiki nao.
Rais Kikwete alisema madaktari lazima watambue pia
kwamba ajira zao wanaziweka hatarini kwani mfanyakazi hana kinga ya kutofukuzwa
kazi na mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria.
"Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa
kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha
yao, kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.
Lazima watafakari kwa hayo wafanyayo," alisema.
Hoja za madaktari
Rais Kikwete alisema katika mambo 12 ambayo
madaktari waliyawasilisha pande zote mbili zilifikia mwafaka na kukubaliana kwa
pamoja kwa mambo saba.
Alitaja la kwanza ni kuhusu usafiri wa kwenda na
kurudi kazini ambalo limeshashughulikiwa.
Alisema jambo la pili, ni madaktari kupatiwa Green
Card za Bima ya Afya ambalo Serikali na Wizara ya Afya zimechukua hatua za
utekelezaji wake.
Jambo la tatu, alilitaja Rais Kikwete kuwa ni hatua
za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya ambalo
tayari Serikali imechukua hatua.
"Uongozi wa juu wa wizara umebadilishwa na
sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajabisha hata Waziri mpya wa Afya
alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema
hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na kamati yake kwa miezi mitatu bila ya
mafanikio," alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa, jambo la nne
walilokubaliana ni viongozi kuwalazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje suala
ambalo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewaeleza madaktari wazingatie maadili ya
kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe
kiongozi.
Alisema jambo la tano ambalo pande zote mbili
zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa.
"Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa
wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala
na Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa
wamerudi Muhimbili," alisema.
Rais Kikwete alisema jambo la sita ni kuhusu mapendekezo
mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya ambalo
Serikali imeliafiki.
Rais Kikwete alisema jambo la saba, ambalo pande
zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.
No comments:
Post a Comment