Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na
kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu
wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo
mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la
pili ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji
Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa
mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43
za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego,
Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti hao,
walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi
yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi
Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa
Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi,
Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro
kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana
kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia
ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini ambako
wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa
maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia
Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako
walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia
Chitego. Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo
kwa kukosa hewa.
Tukio la Chitego,
Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza
kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi cha takriban miaka 10 sasa
kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati
ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa.
Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500
tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi wa watu
hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na Bangladesh.
Wahamiaji haramu
wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo wanaotumia nchi
kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo
wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa
Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli
zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali wao ni wapita
njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa
mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa
watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote
wanazopitia mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao
ili wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu
vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji walipobuni
njia za kuwasafirisha kama mizigo. Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na
matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo. Usafiri wa
aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na
vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile
vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi
Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012
nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuzungumzia tukio la
Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na
wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo
kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa
waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba
kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa kielekeze
sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa
nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika
ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari
nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu
ushirikiano huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja
kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha
utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi
hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri
walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa
taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali
wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na
Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia
tatizo hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na ushirikiano ulioonyeshwa
na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia suala hili.
Mgomo
wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu
mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar
es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo
wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la
mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa
Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza ya
majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea matumaini yangu kuwa mgomo ule
utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa
na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa
kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi,
madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye mazungumzo na
Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi,
2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama
cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
(Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja
na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano
yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi,
2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza
kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10
Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano
kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika mazungumzo hayo hoja au madai
12 ya madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1.Posho ya kuitwa kazini
(on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2.Posho ya kufanya kazi
katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3.Madaktari wapatiwe
nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
4.Posho ya kufanya kazi
katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5.Madaktari walipwe
posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6.Madaktari wanaoanza
kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7.Madaktari wapatiwe
Green Card za Bima ya afya.
8.Hatua za kinidhamu
zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9.Viongozi wa Kisiasa
kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.Madaktari
waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.Huduma za afya
ziboreshwe nchini.
12.Posho ya uchunguzi
wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12
pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. La
kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza
kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka
2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au
pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie
fursa hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo
hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za
utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji
Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya
mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa
juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la
kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja
walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na
Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya
kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba maelekezo ya
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao
na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili,
walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa
nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili
mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza sana bajeti
ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi
trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na
elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.
Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya
Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma. Na kazi
inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda yake
yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa
upande wa ubongo na mishipa ya fahamu. Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya
madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku
za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi
wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari
waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani
kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na
Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa
wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari
kuhusu kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na
mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya
Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango
vya ubora wa madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na
yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya
uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo,
Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi
kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa
wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu
ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya
mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi.
Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya
kazi katika mazingira hatarishi. Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada
zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na
fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali
imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa watumishi wa
umma wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa
kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa
wahusike. Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe
kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
Jambo la pili ambalo
wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi. Serikali imekiri wajibu
wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa
kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi
wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40
katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo
madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya
hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya
kupewa nyumba. Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia
30 ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona vigumu
kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine wote wa
umma.
Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya
kufanya kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo
baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma hivyo
hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka
utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili hiyo,
Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia
watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea
posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali
imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya kufanya
uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi waliopo na gharama
zake.
Madaktari hawajakubali
kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.
Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo
yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira
halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa
na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa
kazini (on call allowance). Kwanza sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali
kuongeza posho hiyo. Tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi
10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi
20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi
15,000/= kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo
kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa upande
wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10
ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo
haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa
hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari
kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale
pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo
muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu mshahara wa
kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/=
wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake
wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama
ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa
kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi
1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye
kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo ndiyo mlolongo wa
mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya mazungumzo yenyewe.
Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha
Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko
hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao.
Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT
aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano
kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi
waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
Baada ya majibu yale ya
madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari walikwenda kwa
Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi kama sheria
inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lifikishwe
Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi. Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu
kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo
kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani
suala lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za
Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha
suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa. Mahakama Kuu
ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais
wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya
MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa.
Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama.
Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye
hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja na rai
hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake kusitisha mgomo.
Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume
cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na
wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria ambao pia
haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari. Viongozi wa MAT na
wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao
isivyostahili. Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari wakatambua kuwa
wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana
Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka
hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki
mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia,
hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha yao kwani
hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali. Lazima
watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno
niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha mishahara na maslahi ya
wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala
(CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa
nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo. Kwa
kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi
hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa
wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni mwa
wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na
watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya. Tena nadiriki kusema madaktari
tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo
kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa
asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005,
mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/
2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha
mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/= wanazolipwa sasa.
Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine wenye
shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa
kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na ukweli kwamba
bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini. Lakini inaonekana
juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza
kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao wa kulipa. Kwa sasa
hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi
3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari
anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho
hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini
kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo
basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa
mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi
hicho. Nasi tutamtakia kila la heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize
kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu
ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa
anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya
kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka
kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa
mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa kazini
maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka za ajira
zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea
kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa.
Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari
aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa
kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini
na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia
kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo
madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo
kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa
hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana
mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa
wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya
tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu
kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi ya
mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa
mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya
bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za
maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13. Hivyo,
hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.
Suala
la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza
hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko
yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt.
Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa
na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.
Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la
kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali
nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi nimeshangazwa sana na
hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa
mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari. Ni
kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya
majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache
maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao
wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza,
mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana. Yapo maeneo
machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana. Hapo
tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria
kusaidiwa. Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka?
Na, kuhusu mgomo,
Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama
ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia
adabu mtu huyo. Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven
Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa
Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa
kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na kwa
niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea
apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa
taifa. Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo
wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa
kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini. Watanzania wenzenu
wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa huruma na upendo na msaada kwa
wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa
Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment