Jul 19, 2012

BOTI YA SKAGIT YAZAMA NA ABIRIA 250, KATI YAO 60 WAHOFIWA KUFARIKI DUNIA

Askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama
wakiwa wamebeba moja ya miili ya watu
waliopoteza maisha katika ajali ya boti ta Stargic

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YATANGAZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO KUFUATIA AJALI YA MELI YA MV. SKAGIT

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za maombolezo.

Dk. Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. 
Katika taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na
pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.

“Nimesikitishwa sana na msiba huu, Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu” Alisema Rais Dk. Shein.

Mbali ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.

Mbali ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya Zanzibar kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo wakati wa jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya majumuisho ya bajeti yake.

Baadhi ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.

Mbali ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika shughuli za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.

Taarifa kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti 30 zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa zao huku wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa katika eneo la Maisara.

Aidha, katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo katika hali nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.

Kazi ya utafutaji na uokoaji zinaendelea asubuhi hii katika eneo la tukio ilikozama meli hiyo umbali wa maili sita Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Boti iliyozama ni kama hii ambayo ni pacha wake.


Spika Makinda achafua hali ya hewa


Kutokana na ajali hiyo, muda mfupi baada ya kipindi cha jioni kuanza, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 47(3) kulitaka Bunge lipitishe Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mafungu bila ya kutolewa ufafanuzi ili wabunge waweze kupata muda wa kujadili tukio hilo.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda alipinga hoja ya Hamad na kutaka Bunge liendelee akieleza kwamba kanuni hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na kwamba tayari ameshawasiliana na waziri husika na kwamba taarifa kamili zitakapopatikana angelitaarifu Bunge.
Baada ya kauli hiyo Spika Makinda aliruhusu shughuli za Bunge ziendelee na kumwita Silima kutoa ufafanuzi wa hoja za wabunge.

Lakini wakati Naibu Waziri huyo akielekea kutoa hotuba yake, wabunge wote wa CUF, Chadema na baadhi wa CCM walitoka nje na kwenda katika Ukumbi wa Msekwa ili kupeana taarifa za ajali hiyo na kupanga mikakati ya jinsi ya kutuma ujumbe wa haraka kwenda Zanzibar kushirikiana na waokoaji.
Ukumbi huo uligeuka kuwa wa maombolezo kwa muda baada ya wabunge wengi kuangua vilio pale walipopewa taarifa rasmi za ajali hiyo.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid alieleza kwa ufupi tukio lilivyo na kwamba wangemwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda awasaidie ndege ya Serikali ili waweze kwenda Zanzibar kujumuika na wenzao katika tukio hilo.

Baada ya Hamad kumaliza alisimama Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye alijaribu kuwatuliza wabunge akisema kuwa, meli inaweza kuzama lakini watu wasipoteze maisha kutokana na kuchukua muda, kauli ambayo ilipingwa na wabunge wengi.Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Ibrahim Sanya alimshutumu Spika Makinda akisema, amekosa hisia na hajui kwamba kuzama kwa meli ni janga la kitaifa.
“Kwa hili hata nikikutana na Spika nitamwambia kweli ameniudhi. Sihitaji ubunge kama hali yenyewe ndiyo hii na tutapiga kura ya kutokuwa na imani na Spika,” alisema Sanya.

Wakati hayo yakitokea, katika Viwanja vya Bunge baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa katika vikundi wakijadili suala hilo, huku wengine wakipinga uamuzi huo wa Spika.

Wakati hayo yakiendelea katika Ukumbi wa Msekwa, Bunge lilikuwa likiendelea kumsikiliza Silima akijibu hoja za wabunge na baada ya kumaliza, Spika Makinda alimwita mtoa hoja, Waziri Nchimbi naye kujibu.Lakini badala yake, alitumia fursa yake kuondoa hoja ya Makadirio ya Matumizi ya wizara yake ili kutoa fursa kwa Bunge kujadili ushiriki wake katika tukio la kuzama kwa boti hiyo.

Dk Nchimbi alitumia Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka mtoa hoja kusimama na kutoa hoja ya kuondoa mezani hoja yake kama kuna jambo la dharura.

“Mheshimiwa Spika, natumia Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka Waziri kusimama na kutoa hoja ya kuondoa mezani hoja yake kama kuna jambo la dharura,” alisema Dk Nchimbi.Dk Nchimbi aliendelea: “Ikumbukwe Mheshimiwa Spika, muda mfupi kabla ya kuingia hapa ndani uliniita mimi na Naibu Waziri ukataka tukueleze hali ya ajali hiyo na kwa wakati huo Kamishna wa Matukio Zanzibar alikuwa eneo la tukio. Sasa basi, kutokana na agizo lako, ni imani yangu kwa muda aliotumia Naibu Waziri unatosha kuendelea kufuatilia jambo hilo.”

Baada ya kutoa maelezo hayo, Wabunge wote 49 waliokuwa wamebaki katika ukumbi walisimama kuunga mkono hoja.
Baada ya hapo, Spika Makinda aliwahoji na kwa kauli moja waliridhia kuahirishwa kwa kikao hicho wakati huo ikiwa saa 11:31 hadi leo saa 3.00 asubuhi, huku akiitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Bunge jana hiyohiyo kujadili suala hilo.

Akizungumza baada ya kikao hicho cha Kamati ya Uongozi, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema, limeamua kufuta kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu na kwamba kikao cha Bunge kitaendelea leo asubuhi kuanzia saa 2:00 kupokea taarifa ya Serikali kisha watajadili mustakabali wa vikao vya Bunge.Kamati hiyo pia iliamua kutuma ujumbe wa wabunge kwenda Zanzibar kuwafarijiwa wale wote walioathiriwa na ajali hiyo.

Ni ajali ya pili
Ajali Mv Spice Islander ambayo ilitokea Septemba 10, 2011 ikitokea Unguja kuelekea Pemba, ilizama kutokana na kuzidisha abiria ambao kwa mujibu wa tume iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo, ilikuwa na abiria 2,470 na mizigo wakati uwezo wake ulikuwa kubeba abiria 600 tu.
Tume hiyo iliyoundwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ilibaini kwamba ajali hiyo ilisababishwa na uzembe, kutofuata sheria na rushwa katika Bandari ya Zanzibar.

Tume hiyo ilipendekeza wahusika wa ajali hiyo kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.
Nohodha wa meli hiyo, Said Abdallah Kinyangite, wamiliki wa meli, watendaji wa Bandari ya Zanzibar walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ambako kesi zao zinaendelea.

Chanzo: Michuzi na Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...