Jun 10, 2012

BOB MAKANI AFARIKI DUNIA, RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI.

Bob N. Makani.
MWASISI wa Chadema na Mwanasheria mkongwe nchini Bob Makani, amefariki dunia usiku katika hospitali ya Aga khan, jijini Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Makani alizidiwa ghafla saa 3: 00 usiku wa kuamkia leo na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alifariki dunia saa 4.15 usiku.

“Amekuwa anaumwa muda mrefu, mara kadhaa akipelekwa hospitali na baada ya muda anaruhusiwa, lakini hii ya sasa alikua nyumbani akazidiwa ghafla wakampeleka hospitali na ilipofika saa 4.15 wakasema amefariki,” alisema Zitto.

Zitto alisema kuwa, suala la wapi utakapozikwa Makani ambaye ni Katibu Mkuu wa Kwanza na Mwenyekiti wa pili wa Chadema, litajulikana baada ya kujadiliana na familia ya marehemu.

“Suala la wapi atazikwa kama ni Shinyanga ama Dar es Salaam, litajulikana baada ya kuzungumza na familia yake, kwa sasa tunashughulika kwanza na kuhifadhi mwili wa mzee wetu,” alisema Zitto.
Zitto alisema msiba wa utakuwa nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Bob Makani akiwa katika Jukwaa.

Kwa siku za hizi karibuni afya yake imekuwa ikizorota na kumfanya kuripotiwa kuanguka mara kwa mara alipokuwa akifanya shughuli zake.

Januari 17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema Regia Mtema, Makani alianguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu.

 Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake

Alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.

Kazi ambazo amewahi kuzifanya serikalini; alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 na elimu yake ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere nchini Uganda.

Ni mzaliwa wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga akitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Makani.

Bob N. Makani enzi za uhai wake.
 ______________________________

RAIS JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitumia  familia ya Mzee Bob N. Makani salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mzee huyo kilichotokea katika Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam. 

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesema kuwa amehuzunishwa na kusikitishwa na habari za kifo cha Mzee Makani ambaye alilitumikia taifa la Tanzania kwa uadilifu na uzalendo katika nafasi mbali mbali alizozishikilia katika maisha yake ikiwamo ile ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

 “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko habari za kifo cha Mzee Makani ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Aga Khan mjini Dar es Salaam. Nilimfahamu Mzee Makani vizuri wakati wa uhai wake. Alikuwa Mzalendo na mtumishi mwadilifu wa umma, sifa ambazo alizithibitisha katika nafasi zote alizozishikilia katika utumishi wa umma ama kwenye siasa.” 

 “Nawatumieni salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, nikiwajulisheni kuwa niko nanyi katika msiba huu mkubwa ambao umewaondolea mpendwa wenu, baba yenu, babu yenu na mhimili wa familia yenu. Napenda mjue kuwa msiba wenu ni msiba wangu. Naelewa machungu yenu katika kipindi hiki, lakini nawaombeeni subira na uvumilivu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya Marehemu Makani. Amen.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...