ILE dhambi ya ubaguzi
ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alionya kwamba huiwezi kuachwa
sawa na kula nyama ya mtu, imeanza kujidhihirisha visiwani Zanzibar, baada ya
kusambazwa vipeperushi vinavyotaka wananchi wenye asili ya Kisiwa cha Pemba kuondoka
Unguja.
Ikiwa ni zaidi ya miaka 17
tangu Mwalimu kutoa onyo hilo, dhambi hiyo ya ubaguzi imeanza kuwatafuna
Wazanzibari katika kipindi ambacho Jumuiya ya Uamsho Mihadhara ya Kiislamu
(Jumiki), inazidi kuhamasisha Wazanzibari kuukataa Muungano.
Wakati kundi hilo la
Jumiki likitaka Zanzibar iwe dola huru, limeibuka jingine linalojitambulisha
kama ‘Watu wa Unguja’ likisambaza vipeperushi vinavyolishutumu kundi hilo la
Uamsho, kwamba wahusika wake ni wananchi wanaotoka Pemba, wakitaka kuvuruga
amani ya Unguja.
Huku wakihusisha baadhi ya
viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), katika
vipeperushi.Hivyo wamemwomba Rais Jakaya Kikwete ashauriane na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wawaruhusu wapewe kisiwa chao cha Pemba.
“Watu wa Unguja tunatoa
ujumbe mahususi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete….
Tumechoka kuishi na Wapemba katika kisiwa chetu cha Unguja, kwani ni watu wasio
na fadhila ya aina yoyote ile,” inasomeka sehemu ya kipeperushi kimoja na
kuongeza:,
“Hivyo, tunakuomba ufanye
mazungumzo na Rais wa Zanzibar ili Wapemba wapewe kisiwa chao cha Pemba.”
Sehemu nyingine inasomeka,
“Hapo siku za nyuma Wapemba walidai kisiwa chao, na ninyi viongozi
mkang’ang’ania kuwa hatuwezi kuvunja umoja. Sasa mnaona hao tayari wameanzisha
chama cha kisiasa cha ‘Uamsho’ kwa kisingizio cha dini.”
Kipeperushi hicho pia
kimedai kwamba, asili ya wananchi wa Pemba ni Wamakonde kutoka Msumbiji wakati
wenyeji wa Unguja wana asili ya Wasegeju kutoka Bara, ndiyo maana wanautaka
Muungano.
“Kila siku mnajenga Unguja
bila ridhaa yetu, nani mtu wa Unguja aliyejenga Pemba? Mnajenga mpaka ndani ya
vyanzo vya maji, tunasema tokeni na hameni mara moja,” inasisitiza sehemu ya
vipeperushi hivyo.
Huku wakilaumu marekebisho
ya Katiba ya Zanzibar na kuitisha kura ya maoni iliyounda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa, wamesema wanahitaji Katiba Mpya ya Zanzibar ili kufuta mfumo huo.
Vipeperushi hivyo pia
vimelaumu kundi la Uamsho kwa ubaguzi kwa wananchi wanaotoka bara na kusema,
kuwa hata Wapemba wako kwa wingi upande huo wa pili wa Muungano.
Wamesisitiza pia kutaka
Muungano kati ya Unguja na Tanganyika bila ya kuihusisha Pemba na kusisitiza:,
“Tunasema tena, sisi watu
wa Unguja tunataka Muungano wa Serikali mbili ya Unguja na Tanganyika bila ya
kuwapo Pemba. Kuwapo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isiyokuwa ya Umoja
wa Kitaifa. Rais wa Zanzibar awe ndiyo Makamu wa Rais wa Muungano.”
Kauli ya Nyerere
Mwaka 1995 akiwa katika
Hoteli ya Kilimanjaro (sasa Hyatt Regency Dar es Salaam) , Mwalimu
Nyerere akielezea nyufa kuu tano zilizokuwa zikiikabili nchi huku wa kwanza
ukiwa ni Muungano.
Mwalimu alionya, “Watu
wazima wameuzungumza Muungano, kwamba tuuvunje au tuendelee. Mtu mwenye akili
hawezi kufikiri Uzanzibari ni fahari: Hana akili. Nje ya Muungano kuna Wapemba
na Waunguja. Mtamaliza kutengana na Watanganyika, halafu mara mtakuta kumbe
sisi si Wazanzibari.”
“Mtajikuta kuna Wapemba na
Waunguja. Wapemba watapata msukosuko kidogo alololo! Mtakuta kumbe kuna
Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama. Hamuwezi mkakaa salama baada ya
kutenda dhambi ya kuwabagua watu wa nchi yenu ileile moja mkawaita wale wao na
hao sisi. Dhambi ile haishii hapo. Ndivyo historia ilivyo; ni sheria ya
historia siyo sheria ya Mwalimu Nyerere.”
Kinyume na onyo hilo la
mwalimu, vipeperushi hivyo vimeorodhesha madai mengine, mojawapo likiwa kwamba
Rais wa Jamhuri ya Muungano awe anapatikana kwa zamu ya kipindi kimoja kila
upande wa Muungano.
Pia kundi hilo limedai
kuwa Waziri Mkuu atoke bara, kila upande uwe na rasilimali zake kama vile
mafuta na madini, ulinzi wa nchi uwe wa pamoja, kuwe na mgawo sawa wa mabalozi
nje ya nchi na kuwa na mgawanyo sawa wa misaada ya maendeleo.
Tamko la Jumiki
Kwa upande wake Msemaji wa
kundi la Jumik, Sheikh Faridi Hadi Ahmad amekosoa vipeperushi hivyo akisema
vimejaa uzushi.
Akizungumza na waandishi
wa habari katika msikiti wa Mbuyuni mjini Zanzibar juzi, Sheikh Faridi alisema
kundi hilo halina uhusiano na Upemba wala Uunguja.
“Hao ni wapuuzi na
wazushi, kama wanataka Wapemba warudi kwao, basi wamwambie na Rais Ali Mohamed
Shein naye aondoke, Yule si ni mwenyeji wa Pemba?” alihoji Sheikh Farid.
Alisema kundi hilo
lilianzishwa kwa ushirikiano na wananchi kutoka Pemba na Unguja kwa malengo ya
kueneza dini na masuala mengineyo.
Kuhusu kujihusisha na
siasa, alisema kuwa Katiba ya Zanzibar na dini ya Kiislamu inaruhusu waumini
wake kushiriki siasa.
“Katiba ya Zanzibar
inasema kuwa kila mtu ana haki ya kushiriki kwenye uongozi wa nchi. Hata Mtume
Muhammad (S.AW), alikuwa ni rais wa eneo lake na alikuwa kiongozi wa dini…
Siasa ni neno la Kiarabu likiwa na maana ya uongozi na uongozi una mambo mengi.
Kwa hiyo tuna haki kabisa ya kushiriki siasa,” alisema Sheikh Farid.
Katika hatua nyingine,
kundi hilo limepinga hatua ya Jeshi la Polisi kuwakataza kufanya mihadhara kama
kawaida yao.
Katika barua yao
waliyomwandikia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Uamsho wamelaumu
hatua ya jeshi hilo huku pia wakimlaumu Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud wakisema kuwa hana mamlaka ya
kuwazuia kufanya hivyo.
Wameipongeza hotuba ya
Rais Ali Mohamed Shein wakisema kuwa, haikukataza mihadhara badala yake
alisisitiza amani.
Kamati ya Bunge
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa amekemea vikali hali ya
machafuko yaliyojitokeza hivi karibuni visiwani humo na kutamka kwamba amani ya
nchi lazima ilindwe kwa gharama yoyote.
Lowassa, aliwapongeza Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kwa kukemea vitendo
viovu vilivyofanywa na baadhi ya watu kisiwani humo pamoja na kulinda usalama
wa taifa.
Akizungumza jana wakati wa
harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika
wa Elerai, Lowassa alionya kwamba amani ya nchi haiwezi kuchezewa na watu
wachache.
“Amani ya nchi italindwa kwa
gharama yoyote ile, hatuwezi kuona amani ya nchi tuliyonayo inachezewa na watu
wachache wenye nia mbaya,” alionya Lowasa.
No comments:
Post a Comment