Jul 1, 2012

TAARIFA KWA WANANCHI NA WAFANYAKAZI WOTE WA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI.

Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikutana tarehe 28 Juni 2012 kujadili na kutathmini hali ya utendaji na utoaji wa huduma  hivi sasa katika Hospitali. Imebainika kwamba utoaji huduma umeathirika  kutokana na mgomo wa baadhi ya madaktari unaondelea kwa takriban wiki moja sasa tangu ulipoanza Jumamosi ya tarehe 23 Juni 2012.

Baada ya tathmini hiyo, Bodi ya Wadhamini imeagiza yafuatayo:

(i) Madaktari waliopo kazini waendelee na kazi kama kawaida;

(ii) Madaktari waliogoma warejee kazini kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na. 76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

(iii) Madaktari waliopo likizo  warejee kazini mara moja. Utaratibu wa kufidia likizo na nauli zao umeandaliwa.

(iv) Uongozi wa Hospitali uwachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi bila sababu za msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za kazi;

(v) Uongozi wa Hospitali ufute mara moja ‘rotations’ za Madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo (interns); na

(vi) Uongozi wa Hospitali uwapange (re-deploy) Madaktari na Madaktari Bingwa waliopo kwenye maeneo yaliyoathirika wakati huu wa mgomo

Aidha, Bodi ya Wadhamini inawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote ambao wameendelea kuwahudumia wagonjwa wetu na wananchi kwa ujumla. Vilevile, Bodi ya Wadhamini inawasihi madaktari na wafanyakazi wote wawe na subira na  waheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo pamoja na maadili ya taaluma zao. 

_________________
Dkt. Gabriel Upunda
KAIMU MWENYEKITI BODI YA WADHAMINI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...