Jul 1, 2012

Dr. Steven Ulimboka alivyotekwa, apelekwa nje kutibiwa.

"NI saa 12:45 asubuhi, bado kiza kimetanda katika eneo hili la Msitu wa  Mabwepande. Mbele yangu namwona mtu akiwa amekaa chini, pembeni ya barabara akiwa amelowa damu mwili mzima."Ninapomkaribia nasikia sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani… naomba msaada jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza Abdallah, mtu wa kwanza kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka baada ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.Abdallah, anasema mara baada kumwona daktari huyo akiwa katika hali hiyo, alijaribu kumkokota kumtoa eneo hilo, lakini alishindwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo. Baada ya hapo, aliamua kusubiri mtu mwingine apite eneo hilo ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi Bunju.Anasema muda mfupi baadaye aliona gari likija mbele yao, akalinyooshea  mkono kulisimamisha. Liliposimama, akamweleza dereva hali aliyokuwa nayo Dk Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa haraka.Abdallah ambaye hadi wakati huo alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia kuwa ni kiongozi wa madaktari kutokana na sura yake kuvimba, anasema walimwingiza katika gari hilo na kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi Bunju.Anasema, Dk Ulimboka wakati huo alikuwa akiendelea kuvuja damu katika baadhi ya majeraha yake huku akiwa hana suruali na kubaki na bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.Kituo cha Polisi BunjuBaada ya kumfikisha kituoni hapo, walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha hapo.Polisi baada kumhoji Dk Ulimboka, aliwatajia namba ya simu ya rafiki yake aitwaye Dk Deo. Walipompigia na kumweleza tatizo hilo, aliamua moja kwa moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kutoa taarifa hizo na hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo akiwamo Mkurugenzi wake, Hellen-Kijo Bisimba.Wawasili kituoniMratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wa kituo hicho, Onesmo Olengurumwa, anasema waliwafika Polisi Bunju saa 3:36 asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amekalishwa kwenye benchi huku damu ikiwa imeganda kwenye majeraha mwilini.Olengurumwa anasema waliwahoji polisi waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia kiasi hicho muda mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili kuwahi kupatiwa matibabu.Olengurumwa anasema polisi walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike.Baada ya muda mfupi, akiwa ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali, Dk Ulimboka aliomba maji ya kunywa akisema ana kiu sana, lakini alipopewa, alikunywa kidogo akashindwa.Anasema wakiwa njiani, alikuwa akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa tukio la kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua."Jamani hawa watu walitaka kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara akisema Dk Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.Maelezo ya Dk UlimbokaBaada ya Dk Ulimboka kuokotwa aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada ya kutolewa msituni na mazungumzo yake yalikuwa hivi;“Nilikamatwa na watu hao usiku wa Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club, Kinondoni na daktari mwenzangu baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja ambaye alidai kuwa anafanya kazi Ikulu.“Kuna jamaa mmoja anafanya kazi Ikulu, kama siku tatu mfululizo alikuwa akitaka kukutana na mimi ila nilishindwa kukutana naye kwa kuwa nilikuwa na kazi nyingi na wakati mwingine mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.Huku akizungumza kwa taabu kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena simu na kumtaka wakutane.“ Jana (Jumanne) alinipigia simu na nikamwambia daktari mwenzangu twende tukaonane naye, wakati huo alitueleza kuwa alikuwa maeneo ya Kinondoni Stereo,” alisema Ulimboka na kuongeza:“Tulipofika maeneo hayo tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye tukamweleza sehemu tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”Alisema kuwa, wakati anakutana na mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.“Kwa kweli siku ile nilivyoonana na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk Ulimboka.Alisema kuwa wakati wakiendelea na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu yule.“Katikati ya maongezi nikaona ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka kuagana alikuwa akizungumza na simu, sijui nini kilikuwa kinachelewesha sisi kuagana,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:“ Ghafla walitokea watu kama watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa mimi.Wakati sijakaa sawa, waliniburuza hadi  barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”Aliongeza, “Nilipowauliza wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi nasumbua sana na nitajua hukohuko, waliniingiza katika gari jeusi, lakini halikuwa na namba. Niliwauliza kosa gani nimefanya? Hawakunijibu kitu na kusema, we twende utajua hukohuko.’’Alisema alipokuwa ndani ya gari hilo watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya Victoria, walichukua sweta nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya ashindwe kuona kinachoendelea ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.“Walinipiga mateke ya mbavuni, wakati mwingine walitumia vitako vya bunduki,  kila nilipokuwa najaribu kuangalia ninapokwenda nilishindwa,” alisimulia  Dk Ulimboka.Alisema kuwa watu hao walimpeleka katika nyumba moja ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha na kuanza kumshambulia kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati huo, wote walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.“Tangu saa sita usiku mpaka saa 9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu, kuna wakati nilijaribu kukimbia wakapiga risasi juu nikasimama na sikuweza kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:“Nilisimama, wakaendelea kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome sindano ya sumu nife au kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa  meno na kucha kwa kolea huku wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari."Alisema kuwa, watu hao walikuwa na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.“Waliniambia kuwa ninajua ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma sindano ya sumu nife au wanikanyage na gari nife,” alisimulia.Dk Ulimboka alisema kuwa awali hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa alidhani ni polisi, lakini baadaye alishindwa kuwaelewa kwani watu hao walimchanganya.“Sikuweza kuwatambua ila naweza kusema ni askari, walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi na wakati huo nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama maeneo ya Mwenge hivi,” alisema Dk Ulimboka.Alisema kuwa baadaye alipoteza fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao kwa mbali.“Nilikuwa sioni na nilipoteza fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari lilitembea muda mrefu, sikujua ni wapi tunakwenda, kumbe ndio huko Mabwepande,” alisema.Alisema kuwa walifika maeneo ya barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.“Waliniburuza na kuniacha huko na muda wa  saa kumi alfajiri ndipo nikazinduka na kuanza kujiburuza kuelekea barabarani ambako nilisaidiwa na mtu mmoja ambaye simtambui,” alisema Dk Ulimboka.

APELEKWA NJE KUTIBIWA.
Wananchi wakiwa wamelizunguka gari la wagonjwa lililompeleka Dk Steven Ulimboka kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kupelekwa nje kwa matibabu.


FEDHA ZA MATIBABU ZAPATIKANA, MADAKTARI WAKATAA MSAADA WA SERIKALI.



MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka amesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.Kusafirishwa kwake kunafuatia hatua ya jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia, kueleza mabadiliko ya hali ya afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa kufanya kazi, hali iliyolazimu pamoja na matibabu mengine, kwenda   kusafishwa damu.

Ingawa madaktari hao wamekataa kuweka wazi nchi anayopelekwa, kuna taarifa kwamba huenda amesafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.

Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) jana makundi mbalimbali ya watu yalifurika wakiwamo wanaharakati na ndugu wa Dk Ulimboka,  waliofika kwa lengo la kumsindikiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Watu hao waliofika hospitalini hapo kuanzia asubuhi, waliendelea kubaki  eneo hilo hadi saa 6:45 mchana msafara ulipoanza.

Dk Ulimboka alisafirishwa kwa gari la kubebea wagonjwa la kampuni ya AAR. Alipofika uwanjani, alisafirishwa kwa  ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, akisindikizwa na watu watatu.

Usiri safari ya Dk Ulimboka

Mapema jana asubuhi, taarifa za kusafirishwa kwake zilizagaa, lakini hapakuwa na mtu wa kuthibitisha safari hiyo na namna atakavyosafiri.

Katika safari hiyo, Dk Ulimboka amesindikizwa na  Dk Pascal Lugajo, kaka yake, Dk Hobakile Ulimboka na mke wake,  Dk Judith Mzovela.

Madaktari watoa tamko

Baada ya Ulimboka kusafirishwa, madaktari walilaani kitendo cha kutekwa na kupigwa mwenzao na kuitaka Serikali itoe tamko juu ya usalama wao.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Edwan Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo na vitisho vya kufukuzwa kazi wanataaluma hao kunakofanywa na Serikali, kumezua  hofu kwa  madaktari wote nchini.

“Tunaamini Serikali inawajibika kwa watu wake, kwa hali ilivyo sasa madaktari wapo kwenye hofu kubwa, tunataka itoe tamko juu ya usalama wa madaktari,” alisema Dk Chitage.

Akizungumzia hali ya Dk Ulimboka, alisema imekuwa ikibadilika mara kwa mara hali ambayo imesababisha kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi .

Chitage alisema kama Serikali ingekuwa na nia ya kuboresha huduma hospitalini hapo ingeweza kununua mashine ya CT Scan ambayo alisema bei yake ni sawa na Toyota ‘Shangingi’ moja.

Kwa upande wao wanaharakati wa haki za binadamu, jana walifika Uwanja wa Ndege wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti wakilaani kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka.

Dk Chitega alisema hadi kufikia jana, walikuwa wamepata fedha zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya matibabu yake. Juzi madaktari hao walisema wanahitaji Dola za Marekani 40,000 (Sh63.2 milioni) ili kumtibu mwenzao nje ya nchi.


Serikali na tiba ya Ulimboka


Wakati mgomo wa madaktari ukiingia siku ya nane leo, Serikali imesema ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya Dk Ulimboka.

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja jana alisema Serikali ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya daktari huyo.

Mwamaja aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa ni haki ya mgonjwa anayepewa rufani ya kutibiwa nje, kugharimiwa na Serikali, lakini
msaada huo wa Serikali ulikataliwa na madaktari hao na kuitaka ikae mbali na matibabu ya kiongozi wao.

“Sisi tulishaanza maandalizi ya kugharimia matibabu yake, lakini madaktari wenyewe walikataa msaada wa Serikali,” alisema Mwamwaja.

Hali yazidi kuwa tete

Kutokana na mgomo huo, uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, umewatimua zaidi ya madaktari 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo.

Hadi kufikia juzi, madaktari 146 walikuwa wamefukuzwa kutokana na mgomo huo katika hospitali za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya Mkoa wa Dodoma.

Mbeya

Habari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya zinadai kwamba, baada ya uongozi wa hospitali hiyo kulazimika kuomba madaktari wengine kutoka hospitali za jijini Mbeya ili kuongeza nguvu, madaktari hao nao wameonekana kutoridhishwa na ombi hilo.

Habari hizo zinasema kwamba, licha ya madaktari hao kupatikana na kwenda hospitalini hapo, walisikika wakilalamika kwamba wao hawapo tayari kufanya kazi sehemu yenye mgogoro na kwamba wao hawawezi kufanywa kama chambo kwa kuhofia usalama wao.

Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo,  Dk Eliuter Samky alikiri kuzidiwa na kusuasua kwa utoaji huduma kwa wagonjwa ambapo alisema kuwa hadi sasa huduma zinazotolewa ni zile za dharura pekee na zile za kawaida wagonjwa wanaambiwa waende Hospitali ya Mkoa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk Seif Mhina, alisema kwa sasa hali inaendelea vizuri kutokana na kujipanga vyema kukabiliana nayo, licha ya kuwa bado kuna tatizo la upungufu wa vitanda hivyo kusababisha wagonjwa kulala chini.

Tanga

Baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya  Bombo, wameitaka Serikali kukaa pamoja na madaktari ili kumaliza tatizo hilo.

Wamesema hali iliyofikia sasa ni mbaya hivyo ni busara pande hizo mbili kukaa meza moja kutatua mgogoro huo bila kujali nani kati yao amesababisha.

Sakina Abdallah ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi ya Gallanis, alisema amesikitishwa na baadhi ya wanasiasa wanaoshabikia kutekwa Dk  Ulimboka.

“Binafsi hali inayoendelea ya mgomo wa madaktari inanihuzunisha sana kwani tunaoumia ni sisi wananchi tunaotibiwa katika hospitali hizi,” alisema Sakina.


Godfrey Jambia ambaye ni majeruhi aliyelazwa katika hospitali hiyo, alisema Serikali inatakiwa kutatua madai ya madaktari hao ili kuwanusuru raia wasio na hatia.

                    
NCCR yaivaa Serikali

Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema Serikali ina maswali ya kujibu kutokana na kushindwa kutatua mgomo wa madaktari nchi nzima.

Chama hicho kimesema Serikali haitakiwi kutumia nguvu ya dola kumaliza mgomo na kuitaka ifute kesi iliyofunguliwa mahakamani ili kukaa meza ya majadiliano na madaktari hao kwa kuwa raia wasio na hatia, wanapoteza maisha kwa kukosa matibabu.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama, James Mbatia, alisema hata kama suala hilo limefika mahakamani, bado linazungumzika kwa kuwa afya za Watanzania zinawahusu wote.

“Hivi Serikali inashindwa kuliondoa jambo hilo mahakamani na kukaa meza moja na madaktari kumaliza tatizo hili..., katika hili lazima tuseme, yaani watu wanakufa tukae kimya, haiwezekani hata kidogo,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Ubabe hauwezi kuingizwa katika uhai wa Watanzania, kama majadiliano ya awali hayakufanikiwa basi wawekwe watu makini watakaosimamia majadiliano haya, hata wabunge wanaweza kusimamia suala hili, mgomo huu hauna itikadi za vyama unawahusu wananchi wote.”



Habari Hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Claud Mshana, Dar, Burhani Yakub,Tanga na Godfrey Kahango, Mbeya

Toka: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...