Fatou Bensouda |
Mwendesha mashtaka Mkuu mpya wa mahakama ya Kimataifa ya makosa ya
jinai ICC, Fatou Bensouda anaanza kazi rasmi tarehe 15.06.2012. Lakini ni
changamoto zipi zilizopo mbele ya mwanamama huyo kutoka Gambia?
"Mara nyingi unafanya kazi katika hali ya muendelezo
wa migogoro, na hali ya usalama wakati mwingine inafanya utekelezaji wa
majukumu usiwezekane bila kuhatarisha usalama wa mashahidi," Bensouda
aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa katika mahojiano maalumu, na
kuongeza kuwa katika mazingira kama hayo, kazi inakuwa na changamoto kubwa.
Fatou alikuwa naibu mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC tangu
mwaka 2004 na pia aliwahi kuwa Mwanasheria mkuu na mshauri wa rais katika nchi
yake ya Gambia. Fatou alisema changamoto kubwa inayomkabili ni kukosa ushirikiano
kutoka kwa baadhi ya mataifa yaliyosaini mkataba wa uanzishwaji wa mahakama
hiyo.
Hatuna Jeshi wala Polisi
Alisema Mahakama ya ICC haina jeshi na wala haina polisi
lakini polisi na majeshi ya mataifa 120 wanachama ndiyo polisi wa ICC na hivyo
wana wajibu wa kusaidiana na mahakama hiyo katika kuwakamata watu kama kiongozi
wa kundi la waasi la LRA Joseph Kony, rais wa Sudan Omar Hassan el Bashir,
lakini akasema kuwa inasikitisha kuona watu hao bado hawajafikishwa mbele ya
sheria.
Alivyoulizwa endapo mahakama ya ICC inavuruga utulivu wa
kisiasa katika nchi kutokana na uchunguzi wa makosa ya jinai, Bensouda alisema
kinyume chake, uchunguzi huo kwa mfano nchini Uganda, umechangia kwa kiwngo
kikubwa kurejesha amani kaskazini mwa nchi hiyo licha ya ukweli kwamba
hawajaweza kumkata Joseph Kony.
Alisema pia katika nchi ya Cote d' Vior, mahakama ya ICC
pia imetoa mchango mkubwa. Tangu mwanzo tulisema tutafanya uchunguzi na
tunangali pande zote zilizokuwa katika mgogoro huu. Kesi ya Laurent Gbagbo
ndiyo ya kwanza....bila shaka kutakuwa na wengine, alisema.
Shutuma za kutumiwa na mataifa makubwa
Bensouda alisema changamoto nyingine inayoikabili
mahakama hiyo ni juu ya shtuma zinazotolewa kwake kuwa inatumiwa na baadhi ya
mataifa kuyaadhibu mataifa mengine huku pia ikilaumiwa kwa kesi ambazo
zimeshindwa kufikishwa mbele yake, akitolea mfano wa Syria, ambayo hata hivyo
alisema haikuridhia Mkataba wa Rome uliyoanzisha mahakama hiyo na hivyo si
mwanachama wa ICC.
Alisema
mahakama hiyo inaweza tu kuingilia kati nchini Syria kama Umoja wa mataifa
utaitaka ifanye hivyo. hata hivyo, alisema kuanza mchakato wa kufungua mashtaka
unaweza kuchukua muda mrefu kwa vile unahitaji uchunguzi wa hali juu kuweza
kuja na ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashataka wahusika, tofauti na inavyoonekana
hivi sasa.
Mwendo ni ule ule!
Bensouda alisema licha ya tuhuma kwamba mahakama ya ICC inawalenga
waafrika pekee, kuwepo kwake katika nafasi ya mwendesha
mashataka mkuu hakutaleta tofauti yoyote na kwamba ataendelea kuonyesha kuwa
ICC inafanya kazi kwa ajili ya, na pamoja na waathirika wa Afrika, kwa sababu
waathirika wote katika migogoro inayofikishwa mbele ya mahakama hiyo ni
waafrika.
Bensouda anamrithi Luis Moreno Ocampo aliejipatia
umaarufu kutokana na kuendesha kesi kadhaa zenye msisimko mkubwa ikiwa ni
pamoja na rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor, aliyehukumiwa hivi karibuni
kwenda jela kwa miaka 50, na kudiriki kumuombea kibali cha kukamatwa, rais wa
Sudan Omar el Bashir, ambaye hata hivyo Umoja wa Afrika unapinga kukamatwa
kwake.
Ocampo alikuwa akishtumiwa kwa kutumia ubabe katika kipindi cha
uongozi wake na inadaiwa wafanyakazi wengi wa juu wa idara yake walilaazimika
kuacha kazi. Lakini Besnouda, ambaye hakukanusha tuhuma hizo dhidi ya bosi wake
wa zamani alisema jambo la muhimu sasa ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
No comments:
Post a Comment