MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa
kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema
atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe auguze
maumivu makali yanayomkabili.
Dk
Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na
silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.
Jana, Dk
Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa
haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali anaendelea
vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.
Dk
Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa
kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
Hata
hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua nini
kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.
Siri
nzito
Akisimulia
mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema, akiwa
katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa
atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye klabu hiyo, lakini,
alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na kuongeza;
"Yaani sikuwa na amani."
Alisema,
"Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa
tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na
yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk Ulimboka)," alieleza na
kuongeza:
"Sijakaa
sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza
kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."
Hata
hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala yake
alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu hali
yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi)
kuzuia watu kumwona.
Daktari
huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji
Uangalizi Maalumu (ICU).
"Kidogo
najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina maumivu
makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu yeyote anayetaka
kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa ni vizuri
nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.
Lakini,
uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka, kuna
ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo tu kwa
sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu ovyo.
Madaktari
wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu tunamlinda wenyewe na
haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo tutahakikisha sisi
wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.
Kiongozi
jopo la madaktari
Katika
hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka,
Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka ana
majeraha mwili mzima.
“Ingawa
kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana, kwani mwili wake
mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”alisema Profesa Kahamba
na kuongeza:
“Aliumia
mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha za vidole
na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno mawili,”alisema.
Alifafanua
kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la
mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na
harakati za kuokoa maisha yake.
Uongozi
wa Moi watoa neno
Uongozi
wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa
bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.
Msemaji
wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali yake
kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari kuingia
ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.
“Mgonjwa
anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua watu
wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi imeshindikana
kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu wake,”alisema Jumaa.
Jumaa
aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa
vazi maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu
wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.
Tamko la
Jumuiya ya Madaktari
Wakati
hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya uchunguzi
iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai mazingira ya tukio
hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.
Katibu wa
Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa wangependa
kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kutoa
taarifa kwa umma.
“Madaktari
kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara,kupigwa na kutupwa katika
Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi
kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi kuhusika ama kutohusika kwa jeshi
hilo,”alisema Dk Chitage.
Chitage
alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya Serikali
kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhu
ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.
“Kumekuwa
na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Dodoma,
Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na itambue kuwa
mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote bali ni kwa Serikali
kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na kuongeza:
“Sisi
madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania wakipoteza maisha kwa
magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika mazingira magumu huku kukiwa
hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa
tiba.”
Mgomo huo
wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo
kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment