Jun 28, 2012

Tuzo ya Deutsche Welle kwa wanablogi bora.

Blogi kwa ajili ya uhuru: Washindi wa tuzo ya mwaka huu ya Blogi inayotolewa na Deutsche Welle-The BOBs, wamekabidhiwa zawadi yao katika kongamano la vyombo vya habari-Global Media Forum mjini Bonn.

"Mnawapatia sauti  jamii ya wachache na mnawapatia uhuru wa kuzungumza. Hii ni changamoto kubwa. Deutsche Welle inataka kuonyesha umuhimu wa kazi yenu na kukupeni moyo muendelee. Mnafanya kazi ya maana." Hayo ndio matamshi yaliyotolewa na mhariri mkuu wa Deutsche Welle bibi Ute schaeffer katika hotuba yake ya ufunguzi kwa washindi sita wakuu wa tuzo ya Blogi.

Hili ni mara ya nane kwa tuzo hiyo ya BOBs kutolewa na Deutsche Welle.

Tume maalum ya kimataifa imewateuwa washindi kutoka jumla  ya mapendekezo 3000 yaliyowasilishwa. Na jumanne (june 26.2012),washindi wote wa tuzo hiyo wakaja Bonn kupokea zawadi yao wakati wa kongamano la vyombo vya habari-Global Media Forum.

Ramani dhidi ya Ubakaji.

Washindi katika kundi la "Matumizi bora zaidi ya Teknolojia kwa manufaa ya jami" ni wale waanzilishi wa "Harassmap"-mtandao wa Misri ambapo wanawake, bila ya kutajwa majina yao, wanaelezea visa vya kunajisiwa kimwili-visa ambavyo huonyeshwa katika ramani, wapi vimetokea. Katika jamii ya Misri watu hawatambui bado wanawake wangapi wanasumbuliwa na visa hivyo.

Zaidi ya watu 500 wanapambana na kuzidi matumizi ya nguvu dhidi ya wakinamama kote nchini Misri. "Hata wanaume wameanza kuhuzunishwa na jinsi baadhi ya wanawake wanavyoathilika." Amesema Rebecca Chiao aliyejiunga tangu mwanzo na mtandao wa "Harassmap".
Boukary Konaté wa Mali akikabidhiwa tuzo yake na
mhariri mkuu wa DW Ute Schaeffer.


Mtandao wa Facebook kutoka Syria-Freerazan-umeshinda katika kundi la "Kampeni bora ya harakati za jamii"-Mtandao huo umewalenga wanablogi wa Syria ambao bado wanashikiliwa jela.Mshindi ni mwanabologi wa kike wa Syria Razan Ghazzawi ambae ameshakamatwa mara kadhaa.Sherry Al Hayek amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya wanabologia wanaochangia katika mtandao huo.

Milioni Kumi wanaujua mwito wa Wang

Sifa kubwa zimetolewa na tume ya Bobs kwa mtandao Kuang Kuang Kuang" kutoka China. Msanii Wang Bo anaonyesha katika kanda za video katuni kuhusu maovu yanayotendeka katika jamii nchini China-kuanzia maziwa ya watoto wachanga yaliyo haribika,kupitia watu kuhamishwa kwa lazima hadi kufikia kutojulikana aliko msanii Ai Weiwei. Tuzo ya Wang inaingia katika kundi la "Mtandao bora wa video."

Tuzo maalum  ya Elimu na Utamaduni ametunukiwa Boukary Konaté wa Mali ambae amepania kuwashawishi wananchi wa Mali wachangie zaidi maoni yao kupitia mtandao wa Internet. Tangu mwaka 2008 Bokary Konaté amekuwa akisimamia mtandao wake alioupa jina "FASOKAN" kwa lugha ya Bambara na kifaransa.Anaelezea jinsi mtu anavyoweza kuingia katika mtandao wa internet kwa msaada wa nguvu za jua na betri ya gari na kuwahimiza wakaazi wa mashambani jinsi ya kutumia mtandao wa Internet.

Tuzo maalum ya Maripota bila ya Mipaka.

Tuzo ya Maripota bila ya mipaka imemuendeya mwanabologi wa Bangladesh Abu Sufian ambae katika bologi zake amekuwa akimulika maovu yanayotendeka katika jamii na hasa hatua za kimabavu za maafisa wa serikali.

Tuzo Bora zaidi.
Mwandishi habari na mshindi mkuu wa
tuzo ya Blogi ya Deutsche Welle,
Arash Sigarchi.
Blogi ya "Dirisha la hofu" ya Arash Sigarchi,imechaguliwa sio tu na wanablogi bali pia na tume ya Bobs kuwa blogi bora zaidi kwa mwaka 2012.Blogi hiyo ni maarufu miongoni mwa jamii ya wairan.Sigarchi amekuwa akifungwa mara kadhaa kwasababu ya blogi zake na mara ya mwisho alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kabla ya kubadilishwa na kuwa miaka 3. Hakuna lakini kilichomfanya abadilishe msimamo wake,si maradhi ya saratani na wala si kifungo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...