May 29, 2012

Zanzibar bado si shwari

Vijana wakiandamana mjini Zanzibar katika Barabara ya Amani wakipinga Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar, jana.

________________________________
VURUGU ZASHIKA KASI, DK NCHIMBI, IGP MWEMA WATOA MAAGIZO MAKALI KWA POLISI
Waandishi Wetu
VURUGU zilizozuka kuanzia juzi katika maeneo kadhaa ya Mji wa Zanzibar na kudhibitiwa, ziliibuka tena jana baada ya vijana kuchoma matairi ya magari barabarani wakipinga kurejeshwa rumande kwa Mhadhiri wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (Jumiki), Sheikh Musa Juma Issa.

Awali, hali ya amani ilikuwa imerejea baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema jana kuongoza mkutano uliojumuisha taasisi mbalimbali visiwani Zanzibar kwa lengo la kutafuta suluhu ya machafuko hayo ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya mkutano huo uliomalizika kwa makubaliano ya kurejea kwa amani, vurugu ziliibuka tena.

Vurugu tena

Kurudishwa rumande kwa Sheikh Issa baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana mahakamani na wenzake wengine sita wakituhumiwa kuhusika na vurugu hizo kulichochea vurugu katika maeneo ya Amani na Mwanakeretwe kwa vijana kuchoma matairi na kufunga mitaa.

Vurugu hizo za vijana zilisababisha polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya vijana hao ambao licha ya kupigwa mabomu walizidi kupiga kelele wakilaani Muungano.

Hadi jana jioni, maeneo ya Chumbuni, Amani, Mwembaladu hali ilikuwa bado tete huku polisi wakifunga barabara kwa ajili ya kudhibiti vijana hao.

Nchimbi, Mwema
Katika mkutano wao, Dk Nchimbi na IGP Mwema walikutana na viongozi wa taasisi za Kiislamu Zanzibar, wawakilishi wa Balozi za Marekani, Norway na Uingereza na kujadili masuala kadhaa ya kuleta amani visiwani humo.

Mkutano huo uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Polisi Zanzibar uliwashirikisha pia maofisa wa sekta ya utalii.

Katika mkutano huo, Waziri Nchimbi alisema suala la kulinda amani ni la wote na akawataka viongozi wa dini na wanasiasa kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa na amani.

“Kwa mwaka mmoja na nusu hivi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imefanya kazi nzuri na tunawapongeza viongozi wote kwa kazi hiyo; Rais Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wake wa Kwanza Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wake wa Pili, Balozi Seif Ali Idd, sasa tusiwavunje moyo,” alisema Nchimbi.

Alisema kuendelea kwa vurugu Zanzibar ni kuonyesha viongozi hao wameshindwa kazi jambo ambalo si sahihi na kwamba vurugu zinaweza kusababisha watalii kuondoka na hasa kwa kuzingatia msimu wa utalii unakaribia.

Nchimbi alisema ujio wake Zanzibar, ulilenga katika mambo matatu muhimu... “Kuwahakikishia Wazanzibari wote kuwa Jeshi la Polisi ni lao na litaendelea kuwalinda na kuwaeleza kuwa viongozi wote wa dini na siasa wana jukumu kubwa la kusaidia kujenga mazingira ya utulivu na amani Zanzibar.”

Aliliagiza jeshi hilo kuwatafuta na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika kufanya vurugu hizo ili haki itendeke.

Kwa upande wake, IGP Mwema aliahidi kushirikiana na viongozi wa taasisi za kidini ili kuendeleza amani na utulivu nchini. Alisema majadiliano na mazungumzo ni muhimu katika kuimarisha amani na kutatua migogoro iliyokuwapo akiahidi kuendelea kubaki Zanzibar.

Taasisi za dini
Kwa upande wake, kiongozi wa Umoja wa Kiislamu wa Elimu, Uchumi na Maendeleo (UKUEM), Dk Mohammed Hafidh Khalfan alilitaka Jeshi la Polisi kuepuka matumizi ya nguvu kubwa wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Alisema taasisi yake pamoja na nyingine za Kiislamu zitatumia juhudi na busara za kuwafanya waumini wake waepuke vitendo vya fujo, kwani vinatoa fursa kwa wahalifu kufanya vitendo viovu.

Hata hivyo, katika kikao hicho Jumiki hawakushirikishwa na hivyo Dk Hafidh kushauri kuwa katika kikao hicho sauti za kundi hilo ni muhimu kusikika kwani baadhi ya mambo wangeweza kuyatolea maelezo.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza), Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin ambaye alifanya juhudi za kuwasiliana na polisi na taasisi nyingine katika kutafuta suluhu za machafuko hayo aliahidi kuendelea na ushirikiano na wadau wote wa amani nchini.

“Sote tuna jukumu la kuhakikisha hali ya amani inarudi Zanzibar na Uislamu hautoi nafasi kwa kufanya uharibifu wala kumdhuru mtu,” alisema Sheikh Muhidin.

Mkurugenzi wa Utalii Zanzibar, Ali Khalil Mirza alisema sekta ya utalii inachangia pato kubwa la taifa kwa zaidi ya asilimia 75, inaweza kutetereka iwapo hali ya utulivu itatoweka visiwani humo na kushauri ushirikiano zaidi kati ya taasisi zote na wadau ili kuimarisha hali ya utulivu.

Marekani yajitosa

Ubalozi wa Marekani nchini umezitaka pande zote inazohusika kufanya kazi pamoja na kuhakikisha amani inapatikana visiwani humo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt ilisema wanajua umuhimu wa mijadala ya kitaifa lakini ni muhimu pande zote zikitumia demokrasia na amani.

“Vurugu hizo zilizotokea kwa siku mbili zilizopita, zinachafua heshima ya Zanzibar ambacho ni kisiwa cha kwanza chenye amani ambacho kilifanya uchaguzi wenye mafanikio ulioleta Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.

Alisema ni muhimu kulinda amani ya Zanzibar ambayo inaruhusu watalii na maendeleo ambayo ni muhimu kwa Wazanzibari na wageni kwa pamoja.

“Tunataka kila mmoja kulinda maisha na mali za watu wasiokuwa na hatia,” ilisema taarifa hiyo.

Kauli za mawaziri
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki alisema vurugu zinazoendelea visiwani Zanzibar, haziwezi kuzuia shughuli za Tume ya Katiba.
Alisema vyombo vya usalama vitahakikisha vinawakamata na kuwashughulikia wale wote waliohusika katika vurugu hizo.
Kairuki alisema mchakato mzima wa uanzishwaji wa tume hiyo ulifuata sheria na hakuna Katiba iliyovunjwa.
Wakati Kairuki akieleza hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alisema hata kama kuna wananchi ambao hawataki Muungano, wanachotakiwa kufanya ni kutoa maoni kwa Tume ya Katiba.
“Wasubiri Tume ya Katiba itakapokuwa ikikusanya maoni ya wananchi waseme kuwa hawautaki Muungano lakini, si vinginevyo,” alisema.
Waziri huyo ambaye alionekana kutotaka kulizungumzia kwa kina suala hilo alihoji iweje aulizwe yeye. Alipoelezwa kuwa yeye ndio waziri anayehusika na masuala ya muungano alisema, “Wasubiri tu.
Kiongozi wa Kanisa
Akizungumzia vuguru hizo, Makamu Mwenyekiti wa Kanisa  Katoliki Parokia ya Mpendae, Geogre Suna alisema vijana hao walivamia kanisa hilo mnamo saa 8:15 kwa kufunga barabara na kisha kuingia ndani na kuanza kuchoma moto mabenchi ya kukalia waumini.
 
“Baada ya vijana kufika kanisani hapa mlinzi pamoja na fundi waliamua kukimbia kuokoa maisha yao, ndipo wakaanza kuchoma moto, kanisani na kuvunja vioo katika nyumba ya paroko,” alisema.
 
Katika eneo la Magomeni, vijana hao walivamia kiwanda cha mbao na kukichoma moto na kuchoma matairi na kuweka mawe makubwa barabarani hali iliyosababisha polisi kuwafukuza kwa kutupa mabomu mengi ya machozi pamoja na kupiga risasi.

Mtwara wanena

Wakazi wa Wilaya ya Tandahimba, Mtwara wamesema ili kumaliza kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni vyema kwa Katiba mpya ikafuta Zanzibar ili nchi hizo zitambulike kwa Tanzania bara na Tanzania Visiwani.
Wakichangia mada katika mdahalo wa kuwajengea uwezo na kuhamasisha wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kutoa maoni pindi Tume ya Katiba Mpya itakapofika wilayani humo, uliofanyika mjini Tandahimba mwishoni mwa wiki wananchi hao walisema ni wakati sasa kwa Katiba kumaliza kero hizo.

“Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kupata jina moja la Tanzania, iweje leo kuwepo Zanzibar? Hapa kunachotakiwa kuwapo ni Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Zanzibar na Tanganyika tulishaziua kwa kuunda Muungano,” alisema Gebra Msuya mkazi wa Tandahimba.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...