Apr 28, 2012

Aua wapenzi wake wawili, awazika ndani ya chumba




17th April 12
Aua wapenzi wake wawili, awazika ndani ya chumba
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia na kumhoji kijana Paul Msalika maarufu kwa jina la “Piya” (24), mkazi wa Mkolani, Jijini Mwanza, kwa tuhuma za kuwaua wanawake wawili na kisha kuwazika ndani ya nyumba alimokuwa anaishi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kimapenzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Deusdedith Nsimeki, akizungumza na NIPASHE jana, alidai kuwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo ya kikatili kwa nyakati tofauti kati ya Machi15 na 27, mwaka huu.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Hajra Seif Swedi anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 45 na 50, aliyekuwa anafanya kazi katika kituo cha mafuta cha GBP kilichopo Igogo, pamoja na Mwatatu Abdalah (46) aliyekuwa anafanya kazi ya kuuza duka eneo la Mkolani Centre.

Nsimeki alidai kuwa, upelelezi wa awali wa Jeshi la Polisi umeonyesha kwamba Piya alifika Mwanza akitokea kijijini kwao Mwabumwa, wilaya ya Bariadi, mkoa mpya wa Simiyu Oktoba mwaka jana.

Alisema baada ya kufika jijini Mwanza, mtuhumiwa alifikia eneo la Ibada Mkolani “A”  na kuishi katika mapango yaliyokuwa karibu na nyumba ya marehemu Hajra ambayo ujenzi wake ulikuwa bado unaendelea na kwamba baadaye mtuhumiwa huyo aliamua kuwa analala katika nyumba hiyo ambayo ilikuwa haina milango wala madirisha kabla ya mwenye nyumba kubaini jambo hilo.

Hata hivyo, alisema kuwa licha ya kubaini kuwa katika nyumba yake kuna mtu huwa analala, Hajra alimruhusu Piya aendelee pengine kwa makubaliano kuwa atakuwa pia akilinda usalama wa nyumba yake.

Kwa mujibu wa Nsimeki, baada ya ujenzi wa nyumba hiyo ya tope kuwa umekamilika ikiwa ni pamoja na kuweka madirisha na milango, hatimaye Hajra alihamia pamoja na wajukuu zake wawili, lakini pia alimkaribisha Piya (mtuhumiwa) waendelee kuishi naye hapo.

Alidai kwamba katika muda ambao waliishi pamoja hatimaye, Hajra na Piya walianzisha uhusiano wa kimapenzi, lakini kwa siri kubwa pasipo wajukuu zake ambao ni wadogo kiumri kujua.

Kaimu Kamanda huyo wa polisi, alidai kwamba, Januari 15, 2012 majira ya usiku, inaaminika kuwa Piya alimtaka tena Hajra kimapenzi, lakini inaonekana mwanamke hakuwa tayari ndipo ukazuka ugomvi uliosababisha Piya ampige Hajra kwa nondo na kumsababishia kifo.

“Baada ya kufanya mauaji hayo, Piya aliamua kumzika Hajra ndani ya nyumba usiku huo huo pasipo watu wengine kujua hadi ilipogundulika Aprili 10, mwaka huu majira ya mchana.”

Kamanda Nsimeki aliongeza kuwa kabla na wakati akiwa tayari amefanya mauaji dhidi ya Hajra, mtuhumiwa Piya ambaye alikuwa akifanya kazi ya kusukuma mkokoteni alikuwa pia na uhusiano wa kimapenzi na Mwatatu Abdalah aliyekuwa amefika Mwanza akitokea nyumbani kwao Biharamulo mkoani Kagera.

Alisema kuwa akiwa jijini Mwanza, Mwatatu alikuwa akifanya kazi ya mama lishe akiwa ameajiriwa na mwanamke anayeitwa Mama Anna eneo la Mkolani.

Alibainisha kwamba nyakati za mchana akiwa katika kazi yake ya kusukuma mkokoteni, Piya alikuwa akienda kula chakula kwa Mama Anna ambako ndiko alikutana na Mwatatu na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.

“Katika kumhoji mtuhumiwa (Piya) inaonyesha alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mwatatu na walikuwa wameshakutana kimwili mara nyingi katika gesti za uchochoroni ambazo nazo tunajaribu kuzichunguza ili kupata taarifa zaidi,” alidai.

Kwa msingi huo, alidai kwamba hata baada ya kuwa amemuua Hajra (mwanamke aliyekuwa akiishi naye), Piya aliamua kumkaribisha Mwatatu nyumbani hapo na kwamba wakati wa kulala usiku ulizuka ugomvi baada ya mtuhumiwa huyo kumtuhumu mpenzi kuwa alimwibia vitenge alivyokuwa amevipata kutoka kwa mwanamke aliyekuwa tayari amemuua.

Kaimu Kamanda alidai kuwa katika ugomvi huo, ndipo Piya alichukua kipande cha nondo na kumpiga nacho kichwani na kumuua papo hapo.

Kamanda Nsimeki alidai kuwa kama alivyofanya kwa mwanamke wa awali, mtuhumiwa huyo aliamua pia kumzika mpenzi wake huyo jirani na mwanamke aliyekuwa amemuua awali.

Alisema kwamba licha ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa aliendelea kuishi katika nyumba hiyo bila wasiwasi, hadi mmoja wa ndugu wa marehemu Hajra alipofika nyumbani hapo kutaka kujua zaidi kuhusu alipo dada yake.

Alisema ndugu huyo wa marehemu Hajra alibaini kuwepo kwa harufu kali ndani ya nyumba ya dada yake, alipofanya uchunguzi zaidi aliona nguo ikiwa imejitokeza kutoka kwenye ‘sakafu’ ambayo haikuwa ya sementi.

Kwa mujibu wa Kamanda Nsimeki, alipoivuta nguo hiyo ndipo akaona kichwa cha mtu akaamua kutoa taarifa Polisi ambao walifika na kufukua mwili wa Hajra na kisha kumkamata mtuhumiwa Piya.

Alieleza kuwa baada ya kuuzika mwili wa Hajra katika taratibu za kawaida, ndugu walirejea nyumbani kwa ajili ya matanga, lakini ilipofika Aprili 14, 2012 waliamua kuhamisha vitu vya marehemu ndipo wakagundua kuwepo kwa mwili wa mtu mwingine uliokuwa pia umefukiwa ndani ya nyumba hiyo.

Alidai kwamba polisi walipewa taarifa na walipokwenda kuufukua ilibainika kuwa ni mwili wa Mwatatu, na mtuhumiwa alipohojiwa alikiri kuhusika na kueleza namna ilivyokuwa hadi kufikia hatua ya kumuua.

Kamanda Nsimeki alidai kuwa kimsingi matukio hayo ni ya kutisha sana, hivyo Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kwenda kijijini alikotokea mtuhumiwa ili kupata historia yake ya nyuma ikiwa ni pamoja na kumpeleka akapimwe ili kujua kama ana akili timamu.

Mtuhumiwa alikamatwa Jumamosi iliyopita na polisi wanaendelea kumhoji.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...