May 20, 2012

Kifo cha Mafisango, Kocha `ashukuru` kafariki Jumatano

20th May 2012


Kocha wa mabingwa wa soka nchini Milovan Cirkovic akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa mchezaji wa Simba Patrick Mafisango.


Kocha wa mabingwa wa soka nchini Milovan Cirkovic,  alisema timu hiyo ingeyumba kama Mafisango angefariki wakati Simba ikiwa katikati ya ligi kuu ya Bara ama mashindano ya klabu ya Afrika.

Mafisango alifariki usiku wa kuamkia tarehe 17 kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku 11 tangu kumalizika kwa ligi kuu ya Bara na tatu tangu Simba iage Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika kwa matuta nchini Sudan.

"Siwezi kuongea mengi... lakini hili ni pengo kubwa kwa Simba, Mafisango alikuwa zaidi ya mchezaji na ameondoka kipindi ambacho bado tunamuhitaji," alisema Milovan na kueleza zaidi:
"Ni pengo kubwa kwa kweli."

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa Mafisango kwenye viwanja vya TCC, Chan'gombe jijini Dar es Salaam, Milovan alisema kifo cha Mafisango ni pigo kubwa ambalo ni ngumu kuzibika kwa haraka.

Alisema kuwa Mafisango ameondoka kipindi ambacho Simba inafurahia ubingwa wake wa ligi kuu ya Bara ambao alitoa mchango mkubwa kufanikisha.

Milovan alisema anaamini msiba huo umemgusa kila mpenda soka hapa nchini na si tu mashabiki wa klabu ya Simba.

Patrick Mutesa Mafisango enzi za uhai wake.



Wakati huohuo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema JK alituma salamu za rambirambi kwa mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage, kuomboleza kifo cha Mafisango juzi.

“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni habari za upotevu wa maisha ya Patrick Mafisango katika ajali ya gari ambayo nimejulishwa ilitokea asubuhi ya kuamkia juzi katika eneo la Chang’ombe mjini Dar es Salaam,” taarifa hiyo ilimkariri JK.

Naye Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kufuatia kifo cha mchezaji huyo, Simba imeifuta jezi namba 30 iliyokuwa ikivaliwa na mchezaji huyo.

'Kuanzia sasa jezi namba 30 haitovaliwa na mchezaji yoyote wa klabu hii kwa ajili ya kuienzi kufuatia kifo cha mchezaji huyu aliyekuwa kipenzi cha klabu yetu kuanzia viongozi, wachezaji na mashabiki," alisema Kaburu.


SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...