Aug 6, 2013

JOHN TENDWA NJE...!!

John Tendwa.
Rais Jakaya Kikwete amemteua Jaji Francis Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa kujaza nafasi iliyoachwa na John Tendwa ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilisema kuwa uteuzi huo ulianza Agosti 2, 2013.

Kabla ya uteuzi huo, Mutungi ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali katika idara ya Mahakama, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

Alikotoka
Historia ya Jaji Mutungi katika utumishi wake mahakamani ilianza mwaka 1989 alipoanza kazi akiwa hakimu, baadaye akateuliwa kuwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Baadaye aliteuliwa na kushika nafasi za Msajili Mahakama ya Ardhi; Hakimu Mfawidhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Msajili Mahakama ya Rufani na hatimaye Jaji katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Kuhusu Tendwa
Tendwa ameachia nafasi hiyo akiwa katika msuguano wa kisiasa na baadhi ya vyama vya siasa, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho hivi karibuni kilitangaza kutokumtambua wala kushirikiana naye.

Katika utumishi wake huo wa miaka 12 tangu alipoachiwa nafasi hiyo na Jaji George Liundi, Tendwa amekuwa akishutumiwa mara kwa mara kwa upendeleo dhidi ya vyama vya upinzani, madai ambayo amekuwa akiyapuuza. Alipotafutwa tena jana kuzungumzia madai hayo hakupatikana kwa kuwa alikuwa nje ya nchi.

Mbali na Chadema, Tendwa ambaye amewahi kukwaruzana na vyama cha CUF na TLP, mara nyingine amekuwa akitoa tishio la kuvifuta vyama hivyo kwa kile alichodai kuwa vinachochea vurugu.

Hali hiyo ilimjengea uhasama baina ya ofisi yake na vyama vya upinzani na kuna wakati aliwahi kutajwa adui namba moja wa vyama vya upinzani na demokrasia.

Mkataba wake
Katika Mkutano wa Bunge la Bajeti, Aprili mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliibua madai kuwa Tendwa alikuwa anaendelea kufanya kazi kinyume na sheria baada ya mkataba wake kumalizika tangu Novemba 2012.
Hata hivyo, Kambi hiyo ilisema haipingi kumwajiri mstaafu kwa mkataba kama ndiye pekee mwenye ujuzi na uzoefu wa kazi husika, lakini haikuwa inaamini kama Tendwa ndiye Mtanzania pekee mwenye sifa hizo.

Wapinzani wafurahia
Kuondoka madarakani kwa Tendwa kumewafurahisha viongozi wa upinzani, ambapo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema chama chake kimepokea kwa furaha taarifa hizo kwa madai kuwa Tendwa alitumia madaraka yake kukikandamiza na kukipendelea chama tawala.

Dk Slaa alisema yeye na chama chake wanashukuru kuondoka kwa Tendwa kabla ya kuiondoa Chadema aliyoapa kuifuta ili kumlinda mwajiri wake ambaye ni Serikali ya CCM.

“Tendwa alikuwa mbaguzi, hakuwa mlezi wa vyama kama sheria ilivyomtaka. Alikuwa akikipendelea chama tawala na kuukandamiza upinzani hasa Chadema. Hakusimamia sheria aliyoapa kuilinda, tunashukuru Mungu amejifuta yeye kabla ya kuifuta Chadema,” alisema Dk Slaa.

“Upo usemi wa Kiswahili kuwa hata kama umefanya mema tisa jambo moja baya linaharibu yote, lakini kwa Tendwa hakuna lolote zuri alilofanya,” aliongeza Slaa.

Dk Slaa alisema mambo mawili mabaya ambayo Chadema hawatayasahau katika utumishi wa Tendwa ni pamoja na kujaribu kuitetea CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru, alipodai kuzungumza na wazee wa mila wakimuonya Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) asifike Arumeru.

“Yote yale alilenga kuitetea CCM ili ishinde, lakini Chadema iliibuka na ushindi.

Jambo lingine alisema ni kujaribu kuizuia Chadema kufanya kazi za kisiasa pale alipowaruhusu kuendelea na mkutano Arusha Mjini na baadaye mkutano huo ukapigwa mabomu na kusababisha mauaji ya wafuasi wao.

“Yale mauaji ya Januari 5, 2011 mkoani Arusha yalichangiwa na undumilakuwili wa Tendwa…mimi niliwasiliana naye mpaka dakika ya mwisho akinisisitiza tuendelee na mkutano, matokeo yake akaja kugeuka. Hakuwa kiongozi huyu bali kibaraka wa CCM.

Dk Slaa alisema Chadema inamhakikishia msajili mpya, Jaji Mutungi ushirikiano wa kila hali na kuwa wanaamini ataingia na kusimamia sheria na siyo kuegemea upande wowote kama alivyokuwa mtangulizi wake.

“Ninamkaribisha Jaji Mutungi. Nina imani amekuja katika kipindi kigumu, tunajua ni mzoefu mwenye uwezo wa kusimamia sheria na ulezi, sisi hatuhitaji huruma, tunataka sheria isimamiwe vizuri.

“Tutampa ushirikiano kikamilifu…asiogope labda Chadema walimkataa msajili, sisi tulikataa mtu, siyo ofisi…Tunaamini ataingia kusimamia sheria na siyo kuegemea upande wowote. Tukiwa na kosa asisite kuonya au kuadhibu, atimize wajibu wake kama mlezi wa vyama na mtetezi wa demokrasia,” alisema.

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema Tendwa hakuwa mlezi wa vyama bali mbaguzi na muuaji wa demokrasia na kuwa kuondoka kwake ni neema kwa demokrasia nchini.

“Tendwa aende tu, kwanza amechelewa. Alitumia madaraka yake vibaya, ndiye aliyenididimiza… alikuwa anavitisho vingi. Nitamsifu Tendwa kwa lipi, msajili gani aliyekuwa akitishia vyama… huyu mtu hakuwa mlezi wa vyama alikuwa muuaji wa demokrasia.

“Aliogopa vyama vyenye nguvu, unakumbuka alishiriki kuua TLP, CUF na sasa Chadema,” alisema Mrema.
Mrema alisema anayo imani kubwa na msajili mpya kwani alikuwa jaji kwenye Mahakama Kuu mahali ambako alikuwa akitenda haki na kwamba wanategemea alivyokuwa akitenda haki katika mahakama vile vile atatenda haki katika nafasi yake mpya.

Naye Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alitofautiana na wenzake na kusema Tendwa alikuwa anafanya kazi ya ofisi yake, kwa nafasi yake na kuwa yanayoonekana kuwa upungufu yalitokana na nafasi na majukumu aliyopewa.

“Kwanza Tendwa hakuondolewa kama aliyefukuzwa, bali amemaliza muda wake, hii ina maana kuwa alikuwa anafanya kazi inayompendezesha mwajiri wake. Yeye hakuwa wa kwanza, kwani kabla yake alikuwa mwingine naye alilalamikiwa,” alisema Ruhuza.

Alisema haamini kuwa Tendwa alididimiza demokrasia kwa sababu hata aliyokuwa akiyasema na kuyafanya hayakuwa na nguvu kisheria.

“Hakuwa na madhara maana hakuwa na mamlaka ya kumwingilia mwanachama mmojammoja… Kauli zake hazingeweza kudidimiza demokrasia maana hakuwa anatumia sheria, alikuwa anaongea kama mtu wa kawaida, maana hata alipokuwa akidai kufuta baadhi ya vyama asingeweza maana sheria ilikuwa haimruhusu,” aliongeza Ruhuza.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...